Jan 25, 2021 02:31 UTC
  • Iran: Vikwazo vya Marekani katika sekta yetu ya mafuta na gesi vimefeli vibaya

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vikwazo vya Marekani katika sekta yetu ya mafuta na gesi vimeshindwa na kufeli vibaya.

Is'haq Jahangiri alisema hayo jana Jumapili wakati alipokagua Maonyesho ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi na Petrokemikali hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, maana ya kuvifelisha vikwazo ni kutoruhusu kukwama wala kusimama miradi ya ndani ya nchi na jambo hilo muhimu limefanyika kwa ufanisi mkubwa katika sekta ya mafuta na gesi ya Iran.

Sekta ya mafuta na gesi ya Iran imeimarika zaidi licha ya vikwazo vya kiwango cha juu mno vya Marekani

 

Amegusia pia vikwazo vikali vya miaka mitatu iliyopita vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, licha ya vikwazo hivyo ambavyo Donald Trump alikuwa anajigamba kwamba hakuna nchi yoyote katika historia iliyowahi kuwekewa vikwazo vya kiwango cha juu kiasi chote hicho, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kufungua kiwanda kikubwa zaidi ya gesi Ghuba ya Uajemi wakati wa vikwazo hivyo na kwa hakika mradi huo ni nembo ya mafanikio ya kazi muhimu zilizofanywa na Iran wakati wa vikwazo vya kiwango cha juu vya Marekani.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amesema, baada ya Marekani kuiwekea vikwazo Iran, zaidi ya dola bilioni 100 za pato la fedha za kigeni la Iran zilipungua. Hata hivyo amesema, Wizara ya Mafuta ya Iran iliweka mikakati imara na kufanikiwa kuvunja rekodi ya usafirishaji nje mafuta na bidhaa zinazotokana na mafuta. Kiwango hicho kilikuwa mara nne zaidi ya vipindi vyote huko nyuma licha ya Marekani kudai kuwa itafikisha sifuri uuzaji mafuta nje wa Iran.

Tags