Jan 25, 2021 07:54 UTC
  • Kamanda: Iran inafuatilia kwa karibu harakati zote za adui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, majeshi ya Iran yanafuatilia kwa karibu harakati zote za maadui.

Meja Jenerali Sayyed Abdolrahim Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameyasema hayo leo asubuhi alipotembelea kituo cha ulinzi wa anga cha Shahid Ismaialian katika mji wa Bandar Lengeh kusini mashariki mwa Iran. 

Meja Jenerali Mousavi amesisitiza kuwa, eneo la kusini mashariki mwa Iran lina umuhimu wa kistratijia katika ulinzi wa anga na kwamba majeshi ya Iran katika eneo hilo yanafuatilia kwa karibu harakati zote za maadui. 

Wakati huo huo Mkuu wa Kamandi ya Majeshi yote ya Iran amesema majeshi ya Iran yamefanya mazoezi 10 makubwa hivi karibuni kote nchini kwa muda wa siku 15 na kuongeza kuwa, mazoezo hayo yamepelekea wananchi wapate furaha huku maadui wakipoteza matumaini.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri ameyasema hayo leo mjini Tehran na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekabiliwa na vitisho mara kadhaa. Ameongeza kuwa rais wa Marekani alitoa vitisho vingi ikiwa ni pamoja na kuutishia mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri

Meje Jenerali Baqeri amesema baadhi ya oparesheni zilizotekelezwa katika mazoezi hayo zilikuwa za mara ya kwanza kabisa katika historia ya mazoezi ya kijeshi nchini.

Aidha amefichua kuwa wakati wa mazoezi hayo, maadui walituma ujumbe kwa njia mbali mbali na kusema kuwa hawana nia ya kuishambulia Iran na kwamba walikuwa na hofu tu kuhusu hatua ambazo waitifaki wa Jamhuri ya Kiislamu wangechukua katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tokea mauaji ya kigaidi ya Shahidi Qassem Soleimani.

Meja Jenerali Baqeri amesema pamoja na hayo, Majeshi ya Iran yako katika hali ya utayarifu wa juu kabisa kwa lengo la kuilinda na kwamba yatendelea kumuonyesha adui uwezo mkubwa yalionao.