Jan 25, 2021 12:46 UTC
  • Dozi zaidi ya milioni 16 za chanjo ya corona kuingizwa nchini Iran hivi karibuni

Mkuu wa kamati ya afya na tiba ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, taratibu zinakamilishwa kwa ajili ya kuingiza nchini dozi 16,800,000 za chanjo ya corona kutoka nchi zenye kuaminika na zilizokubalika.

Hossein Ali Shahriyari, mkuu wa kamati ya afya na tiba ya bunge la Iran ameashiria marufuku ya kuingiza nchini chanjo za corona kutoka Uingereza, Ufaransa na Marekani na kueleza kwamba, kibali kimeshatolewa kwa ajili ya kuagiza chanjo yenye uhakika kutoka nchi zenye kuaminika.

Shahriyari ameongeza kuwa, hadi sasa imeshalipwa rubuni ya dola milioni 53 kwa nchi zilikoagizwa chanjo hizo, ambazo kwa mujibu wa utaratibu, zitawasili nchini mwishoni mwa mwezi huu.

Hayo yanaripotiwa huku Saeed Namaki, Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran akitangaza kuwa, baada ya kuingizwa chanjo ya corona kutoka nje ya nchi, utoaji wa chanjo hiyo utaanza kwa kuhusisha makundi ya watu wenye hali hasasi kiafya na walioko kwenye mazingira hatarishi zaidi.

Mwananchi akipigwa chanjo ya majaribio ya ya corona ya Coviran BARAKAT

Wakati huohuo, Hojjatollah Niki Maleki, mkuu wa kitengo cha habari cha tume ya utekelezaji maagizo ya Imam Khomeini (MA) amesema, baada ya kuchunguzwa hali za watu 21 waliojitolea kupigwa chanjo ya corona iliyotengenezwa nchini , kibali kingine kimetolewa cha kuruhusu kuwadunga chanjo hiyo watu wengine 14 waliojitokeza wenyewe kupatiwa chanjo hiyo kwa ajili ya majaribio.

Awamu ya kwanza ya kuifanyia majaribio kwa binadamu chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 iitwayo COVIRAN Barakat ambayo imetengenezwa na wanasayansi wa Kiirani ilianza kutekelezwa tarehe 29 Desemba 2020.../

Tags