Feb 07, 2021 03:04 UTC
  • Iran yazindua kiwanda cha kuunda makombora ya kubebwa begani + Video

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua kiwanda cha kuunda makombora ya kisasa yanayovurumishwa kutoka begani ikiwa ni katika hatua nyingine ya kuimarisha uwezo wake wa kujihami.

Uzinduzi huo wa jana Jumamosi umehudhuriwa na Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri na Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami. Uzinduzi huo umefanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha jana pia kulizinduliwa kiwanda cha kutegenezaji fueli mango ambayo inatumika kuvurumisha makombora ya kisasa.

Waziri Hatami amesema, makombora yanayorushwa kutoka begani ambayo yameundwa nchini Iran ni kati ya makombora yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na maadui. Amesema makombora hayo ni rahisi kutumiwa lakini yameundwa kwa teknolojia ya hali ya juu sana.

Aidha amesema makombora hayo yameundwa kwa kutegemea teknolojia ya ndani ya Iran kikamilifu bila msaada wa kigeni.

Akiashiria utegenezaji wa fueli mango, Waziri Hatami amesema, kiwanda kilichozinduliwa kitaweza kutosheleza uzalishaji wa makombora yote yanayohitajika humu nchini. Aidha amesema fueli mango huwezesha makombora kurushwa kwa uwezo mkubwa, kwa kasi na kwa masafa marefu zaidi.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri naye amesema viwanda hivyo vilivyozinduliwa jana havina mfano wake katika usalishaji wa makombora ya masafa mafupi kwa ajili ya kujihami angani katika eneo zima la Asia Magharibi.