Feb 17, 2021 02:26 UTC
  • Admeri Khanzadi: India itajiunga na mazoezi mseto ya kijeshi ya Iran na Russia katika Bahari ya Hindi

Kamanda wa Jeshi Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema lengo kuu la mazoezi mseto ya usalama wa baharini katika eneo la kaskazini mwa Bahari ya Hindi ni kufikia usalama jumla kieneo. Aidha ameongeza kuwa, Jeshi la Majini la India sasa litajiunga na majeshi ya majini ya Iran na Russia katika mazoezi hayo.

Admeri Hussein Khanzadi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, tokea mwaka jana jeshi hilo limekuwa likifuatilia ajenda ya kufanya mfululizo wa mazoezi ya usalama baharini katika muundo mseto kwa kuzishirikisha nchi za eneo na dunia.

Ameongeza kuwa, katika mazoezi ambayo yameanza Jumanne, Jeshi la Majini limeshafika katika eneo la mazoezi na pia hivi karibuni Jeshi la Majini la India nalo lijatjiunga na mazoezi hayo mseto.

Admeri Khanzadi ameongeza kuwa, sambamba na matukio mazuri yanayojiri katika Bahari ya Hindi, huko Pakistan nako kunafanyika mazoezi ya 'Aman' yenye lengo la kudumisha amani na usalama baharini ambapo manowari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nazo pia zinashiriki katika mazoezi hayo.

Admeri Hussein Khanzadi

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hivi sasa kunafanyika jitihada katika Bahari ya Hindi ambazo zinaashiria kuwa nchi za eneo, hasa zenye uwezo mkubwa wa kijeshi baharini, zinashirikiana zaidi kuliko miaka ya nyuma.

Aidha amesema kuwa, nukta hiyo inaonyesha kuwepo ustawi wa usalama kwa maslahi ya usalama wa eneo na biashara ya kimataifa. Admeri Khanzadi amesema kuwa madola ya kibeberu ambayo hadi sasa yamekuwa yakieneza ubabe katika eneo yanapaswa kutambua kuwa yanapaswa kuondoka katika eneo kwani hili ni eneo ambalo lina wenyewe na majeshi ya majini ya eneo yana uwezo wa kutosha wa kudumisha usalama. 

Tags