Feb 22, 2021 14:06 UTC
  • Baada ya kubwagwa Trump; Iran na Korea Kusini zafikia makubaliano ya kuhamishiana fedha za kigeni

Gavana wa Benki Kuu ya Iran na balozi wa Korea Kusini hapa Tehran wamekutana katika kikao kilichopendekezwa na balozi wa Korea Kusini, na pande mbili zimefaikiana juu ya namna ya kukabidhiana fedha na matumizi ya vyanzo vya kibenki vya Iran huko Korea Kusini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, katika kikao hicho kumefikiwa makubaliano ya kuhamishwa fedha kutoka vyanzo vya eneo moja na kupelekwa katika eneo jingine. Benki Kuu ya Iran imeitaarifu Korea Kusini kuhusu kiwango cha fedha kinachopaswa kuhamishwa na benki ambazo inabidi fedha hizo zipelekwe.

Balozi wa Korea Kusini nchini Iran amesema kuwa, nchi yake iko tayari kutekeleza hatua zote zinazohitajika kwa ajili ya kutumiwa vyanzo vyote vya kibenki nchini Afrika Kusini na kwamba hakuna mipaka yoyote ya kiwango cha fedha zinazoweza kufanyiwa muamala.

Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani

 

Korea Kusini ilikuwa imekataa kuilipa Iran fedha zake kwa madai ya vizuizi vingi vilivyokuwa vimewekwa na Marekani wakati wa utawala wa Donald Trump.

Gavana wa Benki Kuu ya Iran ameelezea kufurahishwa kwake na hatua ya Korea Kusini ya kurekebisha msimamo wake. Amesema, ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapokeza vizuri hatua za nchi mbalimbali za kurekebisha misimamo yao na kuongeza ushirikiano wao na Tehran, lakini pamoja na hayo Benki Kuu ya Iran itaendelea kupigania na kufuatilia haki zake kisheria ili iweze kulipwa fidia ya hasara zote zilizosababishwa na nchi hizo kukwamisha makubaliano na mikataba yao na Iran kwa madai ya vizuizi vilivyowekwa na Marekani.