Feb 23, 2021 05:01 UTC
  • Kazem Gharib-Abadi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa huko Vienna, Austria,
    Kazem Gharib-Abadi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa huko Vienna, Austria,

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa huko Vienna, Austria, amesema leo Iran imeanza kutekeleza sheria ya "hatua za kistratijia kwa ajili ya kuondolewa vikwazo na kulinda haki za taifa la Iran." Kwa mujibu wa sheria hiyo, kuanzia Februari 23 Iran inasitisha utekelezwaji wa protokali ziada na hivyo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA hautakuwa na idhini kamili ya kukagua vituo vyake vya nyuklia.

Kazem Gharib-Abadi amesema kuanzia saa sita usiku wa kuamkia leo, Iran imesitisha utekelezaji wa hatua za kujitolea zaidi ya mapatano ya usalama wa nyuklia. Iran ilikuwa inatekeleza hatua hizo za kujitolea katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA. 

Balozi huyo ameongeza kuwa vituo vyote vya nyuklia vya Iran vimetakiwa kutekeleza amri hiyo. Vituo vya nyuklia vya Iran sasa vitakaguliwa tu na IAEA kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida katika fremu ya mapatano ya usalama wa kinyuklia maarufu kama 'Safeguards'.

Ikumbukwe kuwa, baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 8 2018, Iran ilijaribu kuyalinda mapatano hayo kwa sharti kuwa upande wa pili nao uyatekeleze. Lakini nchi za Ulaya hazikuchukua hatua zozote za kivitendo za kuyalinda mapatano hayo kama zilivyokuwa zimeahidi.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mnamo Mei 8 2019, kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tokea Marekani ijiondoe katika JCPOA, lilitangaza kuwa, Iran inaanza kupunguza hatua kwa hatua ahadi zake katika JCPOA kwa mujibu wa vipengee 26 na 36 vya mapatano hayo. Hatua hiyo ya Iran ilichukuliwa ili kuwepo mlingano baina ya ahadi na haki zake za kisheria.

Kwa msingi huo kuanzia leo Februari 23, Iran inasitisha hatua za kujitolea kuhusu ukaguzi wa vituo vyake vya nyuklia. Uamuzi huo umechukuliwa katika fremu ya sheria ya 'hatua za kistratijia kwa ajili ya kuondolewa vikwazo na kulinda haki za taifa la Iran'. Sheria hiyo ilipitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran,  mnamo Disemba Mosi mwaka 2020. Kwa mujibu wa sheria hiyo, iwapo Marekani itaendelea kuiwekea Iran vikwazo, basi serikali nayo inashurutishwa kupunguza ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Wiki iliyopita Balozi Gharib-Abadi alitangaza kuwa kupitia barua rasmi, aliifahamisha  IAEA kuhusu uamuzi wa Iran wa kupunguza utekelezaji wa hatua za kujitolea za kushirikiana na wakala huo kuhusu ukaguzi wa vituo vyake vya nyuklia.

Kwa mujibu wa vipengee 26 na 36 vya mapatano ya JCPOA, iwapo upande mmoja katika mapatano hayo utayakiuka, Iran nayo ina haki ya kupunguza utekelezwaji wa ahadi zake katika mapatano hayo.

Tags