Feb 23, 2021 11:58 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la Iran kusimama kidete kuhusu suala la nyuklia

Kama ilivyo hali kuhusu masuala mengine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitalegeza msimamo wake kuhusu kadhia ya nyuklia, na itaendelea kusimamam imara na kutetea suala hilo kwa nguvu zake zote kwa ajili ya kulinda maslahi ya leo na ya kesho ya taifa hili.

Akizungumza hapo jana Jumatatu mbele ya mkuu na wajumbe wa Baraza la Kuchagua na Kusimamia Kazi za Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema matamshi ya hivi karibuni ya Marekani na nchi tatu za Ulaya kuhusu Iran, ni matamshi ya kiburi, ubabe, ubeberu na yasiyo ya kiadilfu na kuongeza kuwa: Matamshi hayo hayatakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuchukiwa zaidi nchi hizo na taifa la Iran. Hii ni pamoja na kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitalegeza msimamo wake wa kimantiki kuhusu suala la nyuklia na itaendelea kusimama imara kadiri ya uwezo wake katika kutetea na kulinda maslahi ya nchi, hata kama hilo litamaanisha kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 60.

Kiongozi Muadhamu amesema: Suala la silaha za nyuklia ni kisingizio tu. Wao wanapinga suala la Iran kuwa na silaha za kawaida kwa sababu wanataka kuipokonya uwezo wake wa kijeshi. Ayatullah Khamenei amesisitiza kwa kusema: Kile kinachoizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia ni fikra na misingi ya Kiislamu ambayo inapiga marufuku kila aina ya silaha, iwe ni za nyuklia au kemikali, ambazo zinaua watu wa kawaida.

Kiongozi Muadhamu akizungumza katika kikao cha baraza hilo

Ameashiria mauji ya umati ya watu laki 2.2 yaliyotekelezwa na Marekani kupitia mabomu ya nyuklia huko Japan na vilevile kuzingirwa watu madhlumu wa Yemen na kubomolewa masoko, shule na hospitali zao kwa mabomu ya ndege za kivita za Saudia na kusema: Mauaji ya raia na watu wasio na hatia ni mbinu inayotumiwa na Wamarekani na Wamagharibi na Jamhuri ya Kiislamu haikubaliani kabisa na mbinu hiyo na ni kwa msingi huo ndipo ikawa hata haifikirii kuunda silaha za nyuklia. Amesema: Kuhusu suala hilo yule damisi wa uzayuni wa kimataifa daima anasema kwamba hatutaruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia. Anapaswa kuambiwa kuwa Jamhuri ya Kiislamu ikiamua kumiliki silaha za nyuklia, si yeye wala wakubwa zake wanaweza kuizuia kuwa na silaha hizo.

Kuna nukta mbili muhimu za kuzingatiwa katika hotuba iliyotolewa jana na Kiongozi Muadhamu.

Nukta ya kwanza inahusu mtazamo mpana wa Iran kuhusu suala zima la nyuklia na matumizi ya amani ya nishati hiyo muhimu. Kuhusu jambo hilo Kiongozi Muadhamu amesema kuwa viwanda vya nyuklia katika siku za karibuni vitakuwa na nafasi muhimu katika uzalishaji wa nishati safi, salama na rahisi ya nyuklia na kwamba ni wazi kuwa nchi inahitajia pakubwa kuwa na uwezo wa kurutubisha madini ya urani. Amesisitiza kuwa nchi haipasi kusubiri hadi wakati huo bali inahitaji kuanza kurutubisha madini hayo hivi sasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake ya baadaye.

Kwa kutilia maanani mwenendo wa kupungua nishati ya visukuku na kuongezeka kasi ya ustawi wa uchumi wa dunia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweka katika mipango yake ya kipaumbele suala la kuimarisha viwanda vya nyuklia kwa ajili ya kujidhaminia nishati safi isiyochafua mazingira.

Nukta ya pili kuhusu suala la mapatano ya JCPOA ni uamuazi uliochukuliwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wa kupitisha sheria muhimu inayopasa kutekelezwa na serikali katika uwanja huo.

Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge)

Kiongozi Muadhamu amesema kuhusu mapatano hayo: Majlisi imepitisha sheria kuhusu suala hili nayo serikali imeikubali na hadi kufikia jana masuala yote yaliyopaswa kutekelezwa yameshughulikiwa na Inshallah, kufikia kesho pia hatua nyingine ya sheria hiyo itachukuliwa.

Ayatullah Khamenei ameongeza kwamba: Wakati Marekani ilipojiondoa katika JCPOA na nchi nyingine pia zikashirikiana nayo amri ya Qur'ani ni kwamba wewe pia unapasa kuachana na ahadi zako. Pamoja na nayo serikali yetu tukufu haikuachana na ahadi zake bali alianza kupunguza taratibu baadhi ya ahadi hizo ambapo kuna uwezo wa kuanza kutekelezwa tena iwapo wao watatekeleza majukumu yao.

Jambo lililo wazi na linalopasa kukubalika na wote ni kwamba elimu na teknolojia ya nyuklia ni suala lililofikiwa kuafuatia juhudi za miaka mingi za wasomi na wanasayansi wa Iran kwa ajili ya matumizi ya amani ya nishati hiyo muhimu na hiyo ni haki halali isiyo na shaka yoyote. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza wajibu wake wote katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA na ni upande wa pili ndio umekataa kutekeleza majukumu yake bali umetoshaka tu kwa kutoa nara tupu zisizo na maana yoyote wala kutekelezwa kivitendo.