Feb 24, 2021 12:03 UTC
  • Rais Rouhani: Serikali mpya ya Marekani ikomeshe haraka ugaidi wa kiuchumi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesea kuwa, serikali mpya ya Marekani inapaswa kusitisha mara moja operesheni za ugaidi wa kiuchumi.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri ambapo sanjari na kutoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia amesema: Sisi tulitia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na tulitekeleza vizuri ahadi tulizokuwa tumejifunga nazo, tukaheshimu saini zetu, lakini nyinyi toeni hukumu nyinyi wenyewe,  kwa hakika hamkutekeleza ahadi zenu si Marekani wala madola mengine.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ukiondoa taifa hili, hakuna nchi yoyote iliyotekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mia kwa mia.

Joe Biden, Rais mpya wa Marekani anayetakiwa na Iran asikariri makosa ya huko nyuma yaliyofanywa na mtangulizi wake

 

Aidha amesema, Iran bado ina nia ya kubakia  kwa nguvu zote katika makubaliano ya nyuklia, lakini jambo lililo wazi ni kuwa, hii leo tupo katika mazingira ambayo, kubakia, uhai na nishati ya makubaliano haya ya nyuklia inafungamana na suala hili kwamba, serikali ya Marekani iachane kabisa na ugaidi wake wa kiuchumi.

Rais Hassan Rouhani amesema pia kuwa, Troika ya Ulaya inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ni wadaiwa wa nchi yetu na kubainisha kwamba, sisi tumefanya subira kwa muda wa miaka mitatu ilhali madola hayo hayajaifanyia chochote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.