Feb 27, 2021 12:28 UTC
  • Shamkhani: Iran haitaruhusu kuhuishwa ugaidi wa kitakfiri katika eneo

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na mataifa mengine yanayopambana na ugaidi katu hayataruhusu kuhuishwa magenge ya kigaidi na kitakfiri katika eneo la Asia Magharibi.

Ali Shamkhani ameyasema hayo leo Jumamosi hapa mjini Tehran katika mazungumzo na Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ambaye anaitembelea Iran kwa mara pili ndani ya mwezi mmoja.

Shamkhani amekosoa harakati na mienendo ya Marekani nchini Iraq na kueleza bayana kuwa, kuchelewa kutekelezwa sheria iliyopasishwa na Bunge la Iraq ya kutimuliwa wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu ndiyo chimbuko la kushadidi migogoro na taharuki katika eneo.

Amesisitizia haja ya kuimarishwa mashirikiano baina ya nchi za eneo kwa shabaha ya kupunguza taharuki na mizozo kupitia njia za mazungumzo.

Shamkhani (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria mauaji ya kizazi ya wananchi wa Yemen yanayofanywa na muungano vamizi wa Saudia kwa msaada na baraka za Marekani na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kutoa ushirikiano wa kuhitimisha vita hivyo vya Yemen.

Kwa upande wake, Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema usalama ni kipaumbele cha kwanza kwa taifa hilo la Kiarabu ambalo kwa miaka mingi linakabiliana na ugaidi.

Mbali na kusisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Iran na Iraq katika nyuga mbalimbali, waziri huyo wa Iraq amegusia azma ya Baghdad kuilipa Tehran malimbikizo ya madeni, baada ya vizingiti vilivyokuwa vinakwamisha hilo kuondolewa. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia) na mwenzake wa Iraq Fuad Hussein 

 

 

Tags