Mar 02, 2021 02:47 UTC
  • Rouhani:  Marekani haina budi ila kuipigia Iran magoti

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kukiri serikali ya Marekani kuhusu kufeli mashinikizo na vikwazo vyake dhidi ya Iran ni mafanikio makubwa kwa taifa la Iran.

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo jana Jumapili wakati alipohutubu katika ufunguzi wa miradi mikubwa ya sekta za mafuta na gesi na kuongeza kuwa: "Kile ambacho tumeweza kukipata ni kutokana na irada, imani na kusimama kidete wananchi."

Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Kwa yakini dunia na Marekani haitakuwa na budi ila kupiga magoti mbele ya taifa la Iran na kuondoa vikwazo vya kidhalimu."

Rais Rouhani ameongeza kuwa serikali mpya ya Marekani hadi sasa imekiri mara nne kuwa 'mashinikizo ya juu kabisa' dhidi ya Iran yamefeli na hayajazaa matunda. Ameongeza kuwa kukiri huko ni mafanikio makubwa katika historia kwani wale ambao wameiwekea Iran vikwazo wanakiri wazi kutofika popote  vikwazo hivyo.

Kituo cha uchimbaji gesi katika eneo la Assaluyeh kusini mwa Iran

Jana Rais Rouhani alishiriki kwa njia ya video katika uzinduzi wa mradi wa kisima kikubwa cha mafuta cha Azar Ilam magharibi mwa Iran ambacho kina uwezo wa kuzalisha mapipa 65,000 ya mafuta ghafi ya petroli kwa siku. Aidha alizindua mradi wa kiwanda cha usafishaji mafuta cha  Kangan kusini mwa Iran na pia mradi wa shirika la petrokemikali la Kian katika eneo la Assaluyeh.

Iran inaendelea kuzindua miradi mikubwa ya mafuta na gesi kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi na hivyo kupelekea vikwazo vya Wamagharibi na hasa Wamarekani dhidi ya nchi hii kufeli.

Tags