Mar 03, 2021 03:55 UTC
  • Mtazamo wa Iran kuhusu matukio ya Yemen; kuangazia viini vya jiostratijia katika eneo la Asia Magharibi

Ismail Baqai Hamaneh, mwakilishi wa kudumu wa Iran katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneza Uswisi amesema kuwa, wale ambao wanapiga ngoma ya vita, wanapaswa kusitisha uuzaji silaha ambazo kimsingi zinatumika kwa ajili ya kuwauwa wananchi wasio na hatia.

Baqai Hamaneh alisema hayo Jumatatu ya juzi katika hotuba yake kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ambapo sambamba na kuashiria misaada ya kifedha ya baadhi ya mataifa kwa mgogoro wa Yemen ameeleza kwamba, jambo hilo halipaswi kutumiwa kama njia ya kufunika ukweli wa mambo ambao ni kuhusika mataifa hayo katika kuibuka na kuendelea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Saudi Arabia ikipata himaya ya Marekani, Imarati na mataifa mengine Machi 2015 ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen sanjari na kuizingira nchi hiyo masikini angani, ardhini na baharini. Hata hivyo Saudia ilifanya kosa kubwa kwa hatua yake hiyo. Kwani kwenda kombo huko kimehesabu kumeufanya utawala wa Riyadh ukwame katika kinamasi huko Yemen. Hata hivyo swali la msingi ni kuwa, hivi kuidhibiti Yemen kuna umuhimu gani kwa Saudia?

 

 

Jibu la swali hili linapaswa kuchunguzwa katika upande wa jiostratijia na jioikonomiki. Yemen ipo baina ya bahari mbili muhimu ambazo zinaifanya nchi hiyo kuwa na umuhimu maalum kistartijia.  Lango Bahari la Babul Mandab kwa upande wa magharibi na mashariki njia zake zinaishia Yemen. Aidha kuwa nchi hiyo baina ya Bahari Nyekundu na Bahari ya India kunaifanya nchi hiyo kuwa karibu mno na njia ya majini ya magharibi na mashariki.

Sababu nyingine ambayo inaifanya ardhi ya Yemen kuwa na umuhimu kistratija ni kuwa kwake karibu na eneo la Pembe ya Afrika.  Hata hivyo kuidhibiti Yemen kumegeuka na kuwa changamoto kubwa kwa Saudia, kiasi kwamba, hata himaya ya kiwango cha juu kabisa ya Marekani haijaweza kuifanya Riyadh ifikie malengo yake ya kibeberu huko Yemen.

Wapiganaji wa Ansarullah ya Yemen

 

Alireza Akbari, mweledi na machambuzi wa masuala ya kisiasa ya Asia Magharibi anasema: Tatizo kubwa la Marekani ni kuwa tata stratijia zake ambapo inapoingia katika kila aina ya makabiliano, huwa haiwezi kupiga vizuri mahesabu ya gharama na hatari za baadaye. Hivyo basi, Marekani na Saudia pia, hazina budi kuwa na tahadhari zaidi.

Matamshi ya Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliyoyatia Jumatatu ya juzi, yanaashiria nukta hiyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Waziri huyo alidai katika hotuba yake katika kongamana la wahisani wa Yemen kwamba, Saudia ina hamu ya kupatikana njia itakayohimitisha vita nchini Yemen. Aidha aliwataka Mahouthi wahitimishe mashambulio yao ya mpakani na yale yanayoulenga mkoa wa Ma’rib ili kuanze mazungumzo ya amani.

Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani

 

Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo, sambamba na kushadidi mapigano katika medani ya magharibi na mashariki mwa Ma’rib na kukaribia jeshi la Yemen na kamati za wananchi kwenye medani za mafuta za eneo la Safer, serikali ya Sana’a imeionya Riyadh kwamba, kama ndege za kijeshi za Saudia na Imarati au waungaji mkono wa muungano uho vamizi zitalishambulia kwa mabomu eneo hilo, jibu la vikosi vya Yemen litakuwa ni kushambulia taasisi za mafuta za Saudi Arabia za ARAMCO.

Kanali Mujib Shamsan, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Yemen anasema kuhusiana na hilo kwamba: Ujumbe muhimu wa mashambulio haya ni onyo la Saudi Arabia kwamba, isije ikafikiria kushambulia eneo la mafuta la Marib.

Kabla ya matukio ya Yemen, madola makubwa ya kieneo yalikuwa yakidhani kwamba, katika mazingira ya mgogoro yangeweza kutwisha stratijia zao katika jiopolitiki ya eneo. Hata hivyo, vita nchini Yemen vimethibitisha kwamba, hizo ni ndoto za alinacha, kwani vikosi vya muqawama vimebadilisha mlingano wa kijeshi katika eneo.