Mar 04, 2021 12:07 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA hayawezi kujadiliwa upya na njia pekee ya kuyalinda na kuyahuisha ni Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Iran.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumanne wiki hii alizungumza kwa simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kusisitiza kuwa, mapatano ya JCPOA yalifikiwa na pande kadhaa za kimataifa zinazojulikana na kupasishwa kwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Rais Rouhani amesema: Kupoteza fursa ya kuyalinda na kuyahuisha mapatano ya JCPOA kunaweza kuifanya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi.  

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN  

Rais Rouhani amesema kuwa, Iran imesitisha utekelezaji wa hiari wa protokali ziada katika fremu ya sheria iliyopasishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) na kwamba, hatua yoyote au msimamo haribifu ndani ya Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia unaweza kuibua changamoto mpya. 

Iran siku zote imetoa ushirikiano mkubwa sana kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ili kuonyesha uwazi katika miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani. Ushahidi wa hili ni ripoti mbalimbali zilizotolewa na wakala huo zikionyesha namna Iran ilivyotekeleza kikamilifu mapatano ya JCPOA katika miaka kadhaa iliyopita. Katika upande wa pili, Iran nayo inataraji kustafidi na haki zake za kutumia teknolojia ya nyukia kwa malengo ya amani, na ikiwa mwanachama rasmi wa wakala wa IAEA, haiko tayari kufumbia macho haki hizo.  

Katika mazungumzo yake ya hivi karibuni na wajumbe wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa, ni marufuku kuunda silaha yoyote inayosababisha mauaji ya raia wa kawaida, sawa iwe ya nyuklia au ya kemikali, na kueleza kuwa: Hata hivyo nchi hii imedhamiria kumiliki nguvu za nyuklia kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nchi, na ndio maana urutubishaji wa urani nchini Iran hautaishia kwenye kiwango cha asilimia 20, na Iran itarutubisha madini ya urani hata kufikia asilimia 60 kulingana na maslahi na mahitaji ya nchi.   

Ayatulllah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  

Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA hadi kufikia mwaka mmoja baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja na kinyume cha sheria kwenye mapatano hayo na imetoa fursa kwa nchi za Ulaya zilizoahidi kuchukua hatua za kufidia taathira mbaya na hasara zilizosababishwa na hatua hiyo ya Marekani ili zitekeleze  ahadi zao. Mwaka mmoja baada ya nchi hizo za Ulaya kushindwa kutekeleza ahadi na majukumu yao, Tehran ilitangaza kuwa, itapunguza hatua kwa hatua utekelezaji wa majukumu na baadhi ya vipengee vya mapatano ya JCPOA kwa mujibu wa vipengee nambari 26 na 36 vya mapatano hayo ya kimataifa ili kuleta mlingano kati ya majukumu na haki zake. Si hayo tu bali Iran pia ililainisha misimamo yake kwa kiwango fulani katika mazungumzo na katika utekelezaji wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, hata hivyo upande wa pili si tu haukuweza kutoa ushirikiano kwa Iran bali Marekani iliwekea Iran vikwazo vipya, na nchi tatu yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pia ambazo ziliahidi kuwa zitaidhaminia Iran maslahi yake ndani ya mapatano ya JCPOA, ama zilishindwa kufanya hivyo au hazikutaka kutekeleza kabisa ahadi na majukumu yao.

Sasa serikali ya Biden inakariri sera zile zile za serikali ya kabla yake na inajaribu kuibua visingizio na mashinikizo ya kiwango cha juu ili kuilazimisha Iran kuketi kwenye meza ya mazungumzo mapya. Marekani inajaribu kuwasha moto katika Bodi ya Magavana wa Wakala wa KImataifa wa Nishati ya Nyuklia kupitia njia ya kupasisha azimio dhidi ya Iran kwa dhana kwamba, kupitia njia hiyo, itaweza kuiburuta Jamhuri ya Kiislamu kwenye mazungumzo. Njia hii pia ilitumiwa huko nyuma kama wenzo wa mashinikizo ya kisiasa, lakini matokeo yake yalikuwa kutatiza zaidi kadhia nzima. 

Joe Cirincione ambaye ni mtaalamu mwandamizi wa  Taasisi ya Quincy amesisitiza kwamba Joe Biden hadi sasa ameendeleza kampeni iliyofeli ya Trump ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran, na kusema: Kuna hatari ya kupoteza mapatano hayo muhimu ya nyuklia iwapo Biden hatobadili mwelekeo wake.