Mar 04, 2021 13:18 UTC
  • Radiamali ya Iran baada ya Troika ya Ulaya kufuta mpango wa kuishitaki Tehran

Sambamba na kuenea habari kwamba nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeachana na mpango wao wa kupasisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA, mwakilishi wa Iran mjini Vienna amesema kuwa, hatimaye mantiki imeshinda.

Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria amesema hayo leo Alkhamisi katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuandika: "Baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kufanya mashauriano na mazungumzo marefu, sasa kumejitokeza cheche za matumaini za kuzuia kuzuka mivutano isiyo ya lazima katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Awali, mashirika mbalimbali ya habari kama vile Reuters, televisheni ya Aljazeera ya Qatar na mwandishi mwandamizi wa Wall Street Journal walikuwa wametangaza kuwa Troika ya Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeamua kuachana na mpango wao wa kuwasilisha azimio lililo dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa IAEA.

Bodi ya Magavana ya IAEA

 

Mwandishi huyo mwandamizi wa Wall Street Journal anayejulikana kwa jina la Laurence Norman alikuwa ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, kuna habari zimeenea kwamba azimio la nchi tatu za Ulaya yaani UIngereza, Ufaransa na Ujerumani dhidi ya Iran, halitawasilishwa tena kwa wakala wa IAEA. Nchi hio zimeamua kurudi nyuma na kulegeza kamba.

Muda mfupi baadaye, Norman ameandika katika Twitter kwamba habari hiyo ni kweli kwani imethibitishwa na duru mbalimbali.