Mar 04, 2021 13:22 UTC
  • Rais Rouhani: IAEA isiwe uwanja wa michezo ya kisiasa

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA usigeuzwe kuwa uwanja wa michezo ya kisiasa na amezitaka nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kutambua kuwa michezo yao ya kisiasa haiwezi kuzisaidia kukwepa majukumu yao ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Mwandishi wa IRIB amemnukuu Rais Hassan Rouhani akisema hayo leo katika sherehe za uzinduzi wa miradi ya taifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran na kuongeza kuwa, maafisa na viongozi wa IAEA wanatambua vyema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na ushirikiano mkubwa na mzuri na wakala huo.

Kabla ya kutangaza leo kuwa zimeachana na mpango wao wa kuwasilisha azimio dhidi ya Iran, nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zilikuwa zimetangaza kuwa zitawasilisha azimio kwa Bodi ya Maghavana wa IAEA kulalamikia kile zilichodai ni kushindwa Iran kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Viongozi wa Troika ya Ulaya (Ujerumani, Uingereza na Ufaransa)

 

Iran iliamua kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano hayo baada ya kuvumilia mwaka mzima tangu Marekani ijitoe kwenye makubaliano ya JCPOA na kuirejeshea Tehran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisubiri muda wote huo wa mwaka mzima ili kuzipa fursa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao na kufidia madhara yaliyosababishwa na hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano hayo ya kimataifa. Hata hivyo nchi hizo za Ulaya zimeshindwa kuheshimu hatua zao na ndio maana Tehran nayo iliaamua kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA kwa awamu 5.

Vile vile Iran imeamua kusimamisha kutekeleza protokali za kujitolea ndani waka la wa IAEA na kubakisha uwajibikaji wa kawaida tu kama wanachama wengine, ikiwa ni njia ya kuhimiza kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa.

Badala ya kutekeleza majukumu yao, nchi tatu za Ulaya zilijifanya kukasirishwa na hatua za Iran za kujibu kutowajibika kwao nchi hizo. Rais Rouhani amezionya zisiufanye wakala wa IAEA kuwa uwanja wa michezo ya kisiasa.