Mar 21, 2021 04:20 UTC
  • Rouhani atoa mkono wa kheri kwa viongozi wa nchi zinazoadhimisha mwaka mpya 1400 (Nowruz)

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewanyooshea mkono wa kheri, baraka na fanaka viongozi na marais wenzake wa nchi kadhaa duniani ambazo zinaadhimisha sherehe za Nowruz (Nairuzi) za kuwadia mwaka mpya wa 1400 Hijria Shamsia.

Katika ujumbe wake huo wa mwaka mpya wa Hijria Shamsia kwa marais na viongozi wa nchi za Afghanistan, Pakistan, Tajikistan, Azerbaijan, Turkmenistan, Armenia, Kazakhstan, Uzbekistan, Uturuki na Iraq, Rais Rouhani amesema anatumai mwaka huu mpya utafungua ukurasa mpya wa furaha, baraka, afya na amani kwa walimwengu wote.

Ametoa mwito kwa nchi za dunia kuongeza kiwango cha ushirikiano ili kwa pamoja ziweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoisumbua dunia kama msambao wa ugonjwa wa Covid-19 na magonjwa ya moyo.

Dakta Rouhani amesema katika ujumbe huo kuwa: Natumai sisi wanadamu, kama vile mazingira, tutazalisha machipuo mapya katika nafsi na roho zetu katika msimu huu mpya, na kwa kuondosha adha ya udhaifu na uzembe tutayapa nishati maisha, fikra na afya za miili yetu.

Mwaka mpya wa 1400 Hijria Shamsia

Jana jioni maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nowruz ambayo huadhimishwa Machi 21 kila mwaka yalifanyika mjini Geneva, Uswisi. 

Maadhimisho ya mwaka huu ya Nowruz yanafanyika katika hali ambayo, dunia inaendelea kukabiliana na janga la Corona ambalo limeshaua watu zaidi ya milioni 2.7 katika pembe mbalimbali za ulimwengu.

Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Tags