Apr 07, 2021 11:34 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, kurahisisha na kuzidisha biashara, kupanua mawasiliano na usafirishaji, kuimarishwa sekta ya utalii na kutumia vyema uwezo wa teknolojia na nguvu kazi hususan vijana ni miongoni mwa vipaumbele vya jumuiya ya D8, na kusisitiza kuwa, Iran iko tayari kwa ajili ya kuwa na ushirikiano mpana zaidi katika nyanja hizo.

Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo leo katika mkutano wa 19 wa mawaziri wa nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya nchi 8 zinazostawi maarufu kama kundi la D8 uliofanyika kwa njia ya intaneti katika mji mkuu wa Kazakhstan, Nur-Sultan. 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria mgogoro usio na kifani wa maambukizi ya virusi vya corona na athari zake mbaya kwa uchumi wa nchi wanachama wa D8 na kusema: Moja kati ya masomo tunayopaswa kupata kutokana na mgogoro huu ni kuona jinsi mgogoro wa afya unavyoweza kusababisha migogoro mingine kama ya kiuchumi, kwenye misaada ya kibinadamu, migogoro ya kielimu, kuzidisha ukosefu wa usawa katika jamii ya kimataifa na kuzisababishia matatizo makubwa zaidi nchi zinazostawi. 

Muhammad Javad Zarif

Dakta Zarif ameashiria vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya taifa la Iran katika kipindi chote cha kasi ya maambukizi ya virusi vya corona na kutaja tukio la kustawi hisia za mshikamano baina ya mataifa mbalimbali na hamu ya kuwepo ushirikiano baina ya mataifa hayo wakati wa migogoro kama somo mazuri ya kujifunza katika kipindi cha maambukizi ya corona. 

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za D8 unaosimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh ambao unahudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Indonesia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Malaysia, Nigeria, Pakistan na Uturuki unatangulia ule wa viongozi wa nchi hizo uliopangwa kufanyika kesho.