Apr 08, 2021 02:35 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, leo tunashuhudia mwanzo mpya wa kuhuishwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Akizungumza Jumatano mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri, Rouhani amesema nchi zote ambazo zinafungamana na mapatano ya JCPOA zinakutana Vienna Austria.

Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Leo kunasikika sauti moja ambapo wale wote walioafiki mapatano haya ya nyuklia wamefikia natija kuwa, hakuna mkondo bora  kuliko ule ulioainishwa katika mapatano ya JCPOA na hakuna njia nyingine isipokuwa kutekelezwa kikamilifu JCPOA. Hayo ni mafanikio makubwa kwa taifa la Iran."

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa, ni fahari kubwa kwa taifa la Iran kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, pamoja na kuwepo masaibu na mashinikizo ya vita vya kiuchumi sambamba na vikwazo vikali zaidi, nchi imeendeshwa kwa njia nzuri ambapo si tu marafiki bali hata maadui wanakiri kuhusu kufeli sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mafanikio haya yamepatikana kutokana na mapambano na muqawama, kusimama kidiete wananchi na uongozi wenye busara wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rouhani amesisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unafuatilia malengo ya amani na dunia nzima sasa inafahamu ukweli huo. Ameongeza kuwa, Iran katu haitaki kufuatilia shughuli za nyuklia zisizo za amani. Aidha amesema iwapo nchi zingine katika mapatnao ya JCPOA zitatekeleza ahadi zao katika mapatano hayo, Iran nayo pia itaanza tena kutekeleza ahadi zake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran ameashiria kukaribia siku ya kitaifa ya teknolojia ya nyuklia na kusema: "Tarehe 10 Aprili tutakuwa na sherehe za kufungua miradi mipya na wanachi wataweza kufahamu ni kipi kilichojiri katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Wananchi wataona makumi ya miradi mipya ambayo itazinduliwa."

Kila mwaka Aprili Tisa huadhimishwa kama Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia nchini Iran. Mwaka huu kutokana na siku hiyo kusadifiana na Ijumaa, itaadhimishwa Jumamosi Aprili 10.

Tags