Apr 08, 2021 07:48 UTC
  • Zarif: Kipaumbele kikuu cha kwanza cha Iran ni majirani zake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, safari yake nchini Kazakhstan ilikuwa na mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa, kipaumbele kikuu cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuishi kwa salama na kwa ushirikiano bora na majirani zake.

Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, Kazakhstan ilikuwa nchi ya tatu ya ziara yake ya kidiplomasia na nchini humo ameonana na Rais Kassym-Jomart Tokayev wa nchi hiyo na waziri mwenzake wa mambo ya nje, Mukhtar Tileuberdi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, nchi mbili hizi zina malengo mengi ya pamoja yakiwemo masuala ya usalama na utulivu wa eneo hili pamoja na kupambana na silaha za nyuklia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapigania haki za wanyonge kote ulimwenguni

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif yuko katika ziara ya kikazi ya kuzitembelea nchi nne za Asia ya Kati za Uzbekistan, Kyrgyzstan, Kazakhstan na Turkmenistan.

Siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Mohammad Javad Zarif zimesimama juu ya msingi wa mazungumo, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, ushirikiano wa kieneo wa kutatua masuala muhimu yakiwemo ya usalama na kutoruhusu madola ajinabi kuingilia masuala ya eneo hili kwani inaamini kuwa madola hayo ya kinyonyaji hayazipendelei kheri nchi za eneo hili.