Apr 08, 2021 13:16 UTC
  • Rouhani: Iran ina fakhari kuwa imejitosheleza katika sayansi na teknolojia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua ambazo zimechukuliwa nchini kufukia kujitosheleza katika sekta mbali mbali za sayansi na teknolojia hasa sekta ya afya.

Akizungumza leo Alhamisi wakati wa kuzinduliwa miradi mitano ya kiteknolojia, Rais Rouhani amesema:" Ni fakhari kwetu kama Wairani kuwa tunajitosheleza hatua kwa hatua katika sketa mbali mbali za sayansi na teknolojia, hasa sekta ya afya, ambayo ni muhimu sana kwetu.

Rais Rouhani amesema uhasama aliokuwa nao rais aliyeondoka wa Marekani Donald Trump dhidi ya Iran ulikuwa sawa na vita vya silaha za sumu au vita vya nyuklia. Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Wakati wa janga la COVID-19 Trump aliendeleza hatua zake dhidi ya Iran na hakujali kuwa watu wa Iran walikuwa wanakabiliana na janga hatari na hata alizuia nchi hii kununua dawa na chanjo". Amesema hata leo serikali mpya ya Marekani inakiri kuwa Trump alifanya kosa na kwamba sera zake za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran zilifeli.

Rais Rouhani amesema dunia nzima leo inakiri kuwa, malengo ya Marekani ya mashinikizo ya juu dhidi ya Iran yamefeli kabisa.

Aidha amesema maadui walikuwa na dhana potovu kuwa wangeweza kusambaratisha uchumi wa Iran na kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu lakini wamefeli. 

 

Tags