Apr 10, 2021 11:10 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna: Njia pekee ya kunusuru mapatano ya JCPOA ni kuondoa vikwazo vyote

Kikao cha Pili cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kimemalizika huko Vienna na pande mbili ziimeafikiana kuendeleza mazungumzo hayo mahsusi kwa lengo la kuandaa faharasa ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuodoa vikwazo na pia kujadili miradi ya nyuklia ya Iran kwa lengo la kuhuisha mapatano hayo.

Duru ya tatu ya mazungumzo ya Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika ngazi ya Manaibu Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 4+1 itafanyika Jumatano ijayo huko Vienna. 

Mazungumzo hayo ya JCPOA huko yana lengo la kupata njia ya  kuondoa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran, na iwapo vikwazo vitaondolewa na kisha kuwa na dhamana na suala hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia itatekeleza tena majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA. Katika mazungumzo hayo ya Vienna hakuna mpango wowote wa kuondolewa vikwazo hivyo hatua kwa hatua, na suala linalojadiliwa ni kuondolewa mara moja na kwa mpigo vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran.   

Njia pekee ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni upande wa pili kuwa irada na azma ya kweli hususan Marekani ambayo inapasa kuondoa vikwazo hivyo bila ya udhuru wa kisingizo chochote. 

Katika uwanja huo, Abbas Araqchi mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran katika kikao cha jana Ijumaa cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA huko Vienna ameashiria azma kubwa ya Iran ya kuendelea kushirikiana kwa dhati ili kuhuisha mapatano hayo na kusema: Suala hilo linategemea irada na azma ya kweli ya kisiasa ya pande shiriki, na kinyume na hivyo hakutakuwa na sababu ya kuendelea kufanyika mazungumzo hayo.  

Abbas Araqchi

Kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo viliwekwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump, ni hatua ya dharura kwa ajili ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA; wakati huo na baada ya kujiridhisha kwamba upande wa pili umetekeleza majukumu yake, Iran itachukua hatua mfano wake ya kutekleza vipngee vyote vya makubaliano hayo. Kwa mfano Iran haipasi kupata shida katika kuuza nje mafuta yake na kupokea fedha za mauzo.  

Kazem Gharib-Abadi ambaye ni mjumbe katika timu ya mazungumzo ya Iran huko Vienna anasema: Kujiridhisha kunakozungumziwa kuna maana ya Iran kufunga mikataba ya biashara ya mauzo ya mafuta, na fedha za mauzo hayo ziingizwe nchini kupitia kanali na njia za kibenki au zitumiwe kwa masuala mengine, na uhamishaji wa fedha hizo utumie njia mbalimbali.

Kazem Gharib-Abadi

Mbali na hayo timu ya mazungumzo ya Iran huko Vienna inajadili maudhui nyingine muhimu ya kwamba je, iwapo Marekani itakiuka tena majukumu yake, Tehran itachukua hatua gani katika majukumu yake yanayohusiana na masuala ya kiufundi.

Kwa kutilia maanani tajiriba ya awali ya mapatano ya nyuklia ya Iran ambayo yalibakia katika nyaraka na karatasi tu bila ya kutekelezwa na upande wa pili, mara hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kupewa dhamana ya utekelezwaji wa makubaliano hayo kivitendo na kuona athari na matokeo yake katika kuondolewa vikwazo vyote.   

Tags