Apr 11, 2021 04:16 UTC
  • Khatibzadeh: Marekani haiwezi kuwa na machaguo mawili kwa wakati mmoja

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisisitiza kuwa, Marekani haiwezi kuwa na machaguo mawili kwa wakati mmoja.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, rais wa Marekani, Joe Biden, asidhani kwamba anaweza kuwa na machaguo mawili kwa wakati mmoja.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, anachotakiwa kufanya Biden ni imma kujiunga na kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA au aendelee kung'ang'ania vikwazo dhidi ya JCPOA na vya kidhulma vilivyowekwa na Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani. Biden hawezi kudai kuwa anaheshimu makubaliano ya JCPOA na wakati huo huo anaendelea kung'ang'ania vikwazo vilivyo dhidi ya mapatano hayo ya kimataifa.

Kikao cha Manaibu Waziri wa Mambo ya Nje wa 4+1 na Iran kuhusu JCPOA mjini Vienna, Austria

 

Wakati huo huo Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema, Tehran imetangaza wazi msimamo wake wa kutaka wahusika wote wa JCPOA waviheshimu kikamilifu vipengee vya makubaliano hayo na kwamba msimamo wa Iran wa kutaka vikwazo vyote dhidi yake viondolewe kwanza ndipo Marekani irejee katika mapatano hayo ni msimamo wa kimantiki kabisa.

Hivi sasa mazungumzo baina ya Iran na kundi la 4+1 lililobakia katika makubaliano ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa, yanaendelea mjini Vienna, Austria.

Katika upande mwingine,  Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana alisema kuwa, kupasishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuliipa uhalali kamili wa kisheria sekta ya nyuklia ya Iran.

Tags