Apr 11, 2021 11:27 UTC
  • Hujjatul Islam Hamid Shahriyari
    Hujjatul Islam Hamid Shahriyari

Dini ya Uislamu imeiweka njia ya uokovu na ufanisi wa mwanadamu hapa duniani na huko Akhera katika mshikamano na kutupilia mbali hitilafu na mifarakano.

Hayo yamesemwa na Hujjatul Islam Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu ambaye yuko safarini nchini Iraq. Sheikh Shahriyari ambaye amekutana na matabaka mbalimbali ya Waislamu wa Iraq, ametilia mkazo suala hilo muhimu na la kistratijia. Vilevile amekutana na maulama na viongozi wa kaumu mbalimbali za Waislamu wa Ahlusunna wa Iraq mjini Baghdad.

Kabla ya safari yake huko Baghdad, Hujjatul Islam Shahriyari alikuwa tayari ametembelea miji mitakatifu ya Najaf na Karbala na kufanya vikao na maulama wa madhehebu za Shia na Suni. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu nchini Iraq, Sheikh Khalid al Mulla. Katika mazungumzo hayo aliashiria njama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Umma wa Kiislamu na mafundisho ya Uislamu na kusema, Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na hatari kubwa ambayo utatuzi wake unahitajia mshikamano na ushirikiano wa Waislamu wote hususan maulama na wanazuoni wa Kiislamu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu nchini Iraq, amesema kuwa suala la kuanzisha mifarakano na hitilafu nchini Iraq ni miongopni mwa mipango ya maadui wa Umma. Ameongeza kuwa: "Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei, hii leo tunahitajia zaidi kuhuisha mradi wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu na umoja wa Umma wa Kiislamu kuliko wakati wowote mwingine."

Maulama wa Kiislamu 

Katika matamshi yake, Ayatullah Khamenei aliweka wazi makundi na mirengo inayozusha mifarakano baina ya Waislamu na kusema kuwa, makundi na mirengo hiyo ndiyo inayotekeleza sera za kuzusha hitilafu katika Umma.

Sehemu kubwa ya makundi hayo haribifu yamepata mafunzo na miongozo kutoka kwenye fikra za kiwahabi na kitakfiri za Saudi Arabia, na fikra hizo sasa zinatumiwa kwa ajili ya kuanzisha vita na machafuko katika nchi za Kiislamu. Mwenendo huu haribifu ni mirathi ya kipindi cha ukoloni ambayo imeathiri zaidi eneo la Magharibi mwa Asia lililotwishwa utawala ghasibu wa Israel. Kwa sababu hiyo Ulimwengu wa Kiislamu hii leo unahitajia zaidi umoja na mshikamano. Katika mazingira haya masomi, wanasiasa na wanafikra wana majukumu magumu na mazito zaidi ambayo iwapo watayatekeleza vyema na ipasavyo wanaweza kuzuia na kubatilisha njama za maadui wa Umma wa Kiislamu.

Katika mkondo huo Sheikh Mahdi Al Samida'i ambaye ni mkuu wa Darul Iftaa ya Iraq anasema: "Ushirikiano mzuri wa Iran na Waislamu wa Ahlusunna kote duniani hususan Iraq na juhudi za kupambana na kundi la kigaidi la Daesh umezuia fitina na njama za maadui wa Umma."

Sheikh Mahdi Al Samida'i

Jambo lenye umuhimu zaidi katika kipindi cha sasa ni juhudi za kulinda maslahi ya Ulimwengu wa Kiislamu na kukabiliana na vitisho vinavyolenga Umma; suala ambalo litasaidia katika kustawisha zaidi ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu. Hili ndilo jambo lililotiliwa mkazo zaidi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu katika safari yake ya sasa nchini Iraq. Hujjatuul Islam Shahriyari amesema kuwa: Kukurubisha pamoja madhehebu za Waislamu ni stratijia ambayo itaimarisha Ulimwengu wa Kiislamu na kuharakisha mporomoko wa madola ya kibeberu kama Marekani.