Apr 12, 2021 11:25 UTC
  • Tukio la Natanz; udharura wa jamii ya kimataifa na IAEA kukabiliana na ugaidi wa kinyuklia

Jumapili alfajiri kulijiri tukio la kigaidi katika mfumo wa usambazaji umeme wa kituo cha urutubishaji urani cha Natanz hapa nchini.

Akizungumzia tukio hilo la kigaidi hivi karibuni, Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kwamba ugaidi wa kinyuklia ambao umetokea katika kituo cha urutubishaji urani cha Natanz ni thibitisho la wazi la kushindwa wapinzani wa ustawi wa kiviwanda na kisiasa wa Jamhuri y a Kiislamu kwa ajili ya kuzuia maendeleo makubwa ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza leo asubuhi katika kikao cha Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) pia ameashiria tukio hilo la Natanz na kusisitiza udharura wa kulindwa vizuri usalama wa taasisi na wanasayansi wa nyuklia katika mazingira haya tata.

Huku akibainisha kuwa maafisa wa kijeshi na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wamesema wazi kwamba hawataruhusu kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vinavyotekelezwa dhidi ya Iran na kwamba sasa wanadhani kuwa wanakaribia kufanikiwa, ameongeza kwamba: Bila shaka Wazayuni watapata jibu lao katika ustawi mkubwa zaidi wa nyuklia wa Iran.

Ali Akbar Salehi

Kituo cha nyuklia cha Natanz huko nyuma pia kiliwahi kushambuliwa kimtandao kwa ushirikiano wa Marekani na utawala wa kigaidi wa Israel. Mashambulio hayo yalitekelezwa dhidi ya kituo hicho katika kipindi cha utawala wa George Bush mwaka 2006 na pia yakakaririwa katika utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani. Kutumwa na maadui vipuri bandia na virusi haribifu kama 'stuxnet' katika kituo cha nyuklia cha Natanz wakati wa kufanyika mazungumzo ya nyuklia ya kundi la 5+1 mwaka 2015 huko Vienna Austria ni sehemu ya msururu wa uharibifu ambao umeelekezwa katika kituo hicho na maadui wa Iran.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kanuni za kulinda usalama wa vituo vya nyuklia pamoja na maazio ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, ni marufuku kuchukua hatua za uharibifu na mashambulio ya kimtandao dhidi ya taasisi za nyuklia za nchi nyingine za dunia.

Pamoja na hayo lakini utawala unaotenda jinai wa Isreal na kwa msaada wa washirika wake wa kigaidi unafuatilia hatua za kuibua mgogoro katika eneo la Asia Magharibi (Maqshariki ya Kati). Kwa msingi huo si jambo la kushangaza kuona viongozi wa utawala ghadibu wa Israel wakijihusisha wazi wazi na bila ya aibu yoyote na vitendo vya ugaidi unaodhaminiwa kiserikali. Mashambulio ya kimtandao yanaweza kutekelezwa kwa niaba na wala hakuna haja ya wahusika kubeba dhima ya kuhusika nayo moja kwa moja. Huenda ni kwa sababu hiyo ndipo utawala wa Kizayuni ukaamua kutumia vibaraka wake kutekeleza mashambulio ya aina hiyo dhidi ya vituo vinavyolengwa ili kukwepa kubebeshwa lawama za ugaidi huo wa kiserikali.

Ugaidi huo wa utawala wa Kizayuni bila shaka una mifano mingine mingi iliyo wazi. Shambulio lililotekelezwa na utawala huo dhidi ya kituo cha nyuklia cha Iraq mwaka 1981 ni moja ya mifano ambayo inakiuka moja kwa moja hati ya Umoja wa Mataifa na kuchukuliwa kuwa uchokozi wa wazi dhidi ya nchi inayojitawala. Baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio nambari 487 dhidi ya utawala wa Israel kutokana na shambulio hilo, liliutaka utawala huo wa kibaguzi ukomeshe mara moja mashambulio ya aina hiyo dhidi ya nchi nyingine.

Kirusi cha Stuxnet kilichotumika huko nyuma kuhujumu mpango wa nyuklia wa Iran

Lakini utawala huo ambao unaona kuwa uhai wake unategemea na kufungamana moja kwa moja na mashambulio ya kigaidi, ungali unaendeleza vitendo hivyo vya uharibifu ambavyo vinakiuka sheria za kimataifa. Mashambulio ya mara kwa mara yanayotekelezwa na ndege za kivita za Israel katika ardhi za Syria na Lebanon, ushirikiano wa shirika la ujasusi la Mosad na mitandao ya kijasusi na vile vile makundi mashuhuri ya magaidi katika eneo bila kusahau vitendo vya uharibifu wa kinyuklia, yote hayo ni katika alama za utambulisho hatari na wa kihujuma wa Israel.

Kwa vyo vyote vile, kwa msingi wa sheria za kimataifa, kila aina ya hatua za uharibifu katika taasisi za nyuklia zilizo chini ya usimamizi wa wakala wa nyuklia wa IAEA ni ukiukaji wa wazi wa misingi ya hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za  IAEA na kanuni za kimataifa zinazohusu usalama wa nyuklia duniani. Ni kwa msingi huo, ndipo Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran akasisitiza udharura wa jamii ya kimataifa na wakala wa IAEA kuchukua hatua za lazima ili kukabiliana na ugaidi wa kinyuklia na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki kamili ya kuwachukulia hatua watekelezaji, waamrishaji na wahusika wa moja kwa moja wa tukio la ugaidi wa hivi karibuni katika kituo chake cha urutubishaji urani huko Natanz.