Apr 12, 2021 11:32 UTC
  • Jerusalem Post: Shambulizi dhidi ya Natanz lilipangwa hapo awali

Gazeti la utawala wa Kizayuni la Jerusalem Post limeandika kuwa, hujuma dhidi ya taasisi ya nyuklia ya Natanz nchini Iran lilipangwa siku nyingi zilizopita kabla ya kuanza mazungumzo ya sasa huko Vienna baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kundi la 4+1.

Katika ripoti yake ya leo Jamatatu kuhusu tukio la jana kwenye kituo cha nyuklia cha Natanz, gazeti hilo la Jerusalem Post limeandika kuwa, mipango ya kufanya "hujuma" katika kituo hicho ilifanyika muda mrefu huko nyuma. 

Gazeti hilo limedai kuwa, shambulizi dhidi ya taasisi muhimu ya nyuklia ya Iran huko Natanz lilipangwa muda mrefu kabla ya mazungumzo ya sasa ya nyuklia baina ya Iran na madola makubwa huko Vienna nchini Austria. 

Gazeti la Jerusalem Post limeongeza kuwa, kuna uwezekano kuwa "shambulizi" la Natanz limefanyika kwa shabaha ya kuathiri mazungumzo yanayoendelea huko Vienna. 

Wakati huo huo Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi amesema kuwa, hatua iliyochukuliwa dhidi ya kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz imeonyesha kufeli wapinzani wa maendeleo ya kiviwanda na kisiasa ya taifa hili na kushindwa wale wanaopinga mazungumzo ya Iran kwa ajili kuondolewa vikwazo vya kidhalimu.

Ali Akbar Salehi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani harakati hiyo ovu na imesisitiza haki yake ya kulipiza kisasi dhidi ya upande wowote ulioamuru na kutekeleza kitendo hicho. 

Tags