Apr 13, 2021 03:40 UTC
  • Iran yasitisha mazungomzo kamili na Umoja wa Ulaya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikwazo ambavyo Umoja wa Ulaya (EU) umeweka dhidi ya baadhi ya taasisi na maafisa wa Iran. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema kufuatia vikwazo hivyo, Iran inasitisha kwa muda mazungumzo yake kamili na Umoja wa Ulaya yakiwemo yale yanahohusu haki za binadamu.

Akizungumza Jumatatu usiku, Khatibzadeh amelaani vikali vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya na kusema havifai. 

Mapema Jumatatu, Baraza la Umoja wa Ulaya lilitangaza kuongeza watu wanane na taasisi tatu katika orodha yake ya vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio cha ukiukwaji wa haki za binadamu. Miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa Iran waliowekewa vikwazo ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Hakuna shaka kuwa hatua kama hizo za wanaodai kutetea haki za binadamu zitawapotezea itibari zaidi."

Khatibzadeh amebaini kuwa: "Katika kujibu hatua hiyo, Iran inasimamisha mazungumzo yote kamili ambayo imekuwa ikifanya na Umoja wa Ulaya, yakiwemo mazungumzo kuhusu haki za binadamu na ushirikiano wowote unaotokana na mazungumzo hayo, hasa katika masuala ya ugaidi, mihadarati na wakimbizi."

Aidha amesema Iran pia inatafakiri kuuwekea Umoja wa Ulaya vikwazo na kwamba vikwazo hivyo vitatangazwa hivi karibuni.

Tags