Apr 13, 2021 10:45 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia mjini Tehran; sisitizo la azma ya pamoja ya kupanua ushirikiano wa kistratejia

Sergey Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia Jumannae ya leo Aprili 13 amekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo wawili hao wamejadili na kuzungumzia masuala muhimu ya pande mbili, kieneo na kimataifa.

Mawaziri hao wametiliana saini pia hati ya kuasisi vituo vya kiutamaduni baina ya Iran na Russia.  Safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia hapa mjini Tehran ina umuhimu katika nyanja mbalimbali.

Kazem Jalali, balozi wa Iran nchini Russia sambamba na kuashiria umuhimu wa safari hii na kwamba, viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili hizi wamebadilishanan jumbe muhimu anaamini kuwa, safari ya Lavrov katika kipindi hiki ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuandikia Rais Vladimir Puitin wa Russia barua muhimu na kiongozi huyo wa Russia kujibu barua hiyo na nukta muhimu zilizoko barua hizo ni hatua ambayo inaweza kuhesabiwa kuwa mwanzo wa kutekelezwa kivitendo matakwa ya viongozi hao wawili yaliyopo katika barua hizo.

Uhusiano wa Russia na Iran kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa kiuchumi na jiopolitiki ya nchi mbili unahesabiwa kuwa ni wa kistratejia. Aidha nchi mbili hizi zina mchango muhimu na athirifu katika kudhamini usalama na kuimarisha mitazamo ya pamoja ya kiulinzi katika kukabiliana na vitisho vya pamoja.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Russia wakitiliana saini mikataba ya ushirikiano (13/04/2021)

 

Fauka ya hayo uwezo uliopo katika uga wa Bahari ya Gaspian, majimui ya Eurosia na korido ya kimataifa ya Kaskazini-Kusini; ni mambo ambayo yameongeza maradufu umuhimu wa uhusiano wa Iran na Russia.

Kwa kuzingatia hayo, kunazungumziwa maudhui ya kimhimili na kistartejia katika malengo ya uhusiano wa Iran na Russia:

Jambo la Kwanza; kuandaliwa mazingira ya kupatikana uhusiano wa muda mrefu katika fremu ya kambi zenye nguvu za kisiasa, kiuchumi na kiusalama. Uhusiano wa kiwango hiki umepatikana pia kwa nchi kama ya China.

Jambo la Pili; kumarisha uhusiano wa kisiasa wa pande kadhaa. Vitisho na changamoto za pamoja za Iran na Russia katika uga wa kieneo na kimataifa, zinapelekea kuweko udharura maradufu wa mitazamo ya pamoja ya kuyapatia ufumbuzi matatizo na kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani.

Vladimirov Sayev, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mitazamo ya Pamoja cha Eurosia anasema: Iran na Russia zimo katika mashinikizo makubwa kabisa ya vikwazo vya Marekani kwa sababu hazitaki kusalimu amri mbele ya siasa za kibeberu za Washington.

Dakta Muhammad Javad Zarif akimkaribisha mgeni wake Sergey Lavrov Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia

 

Mchambuzi huyo wa mambo wa Russia anaamini kuwa, jambo hili kwa Tehran na Moscow lina maana ya hatima na maslahi ya pamoja katika uga wa kimataifa na vile vile ni fursa kubwa kabisa kwa ajili ya kutiliana saini hati za makubaliano ambazo zitadhamini umoja na mshikamano wa nchi mbili.

Jambo la Tatu; ni kuwa wa kistratejia uhusiano wa Iran na Russia katika masuala muhimu ya kieneo kama vita dhidi ya ugaidi, kusaidia kupatia ufumbuzi migogoro na mizozo ya kieneo kama ya Syria, Yemen na Afghanistan.

Mbali na mambo yaliyoashiriwa, umuhimu wa safari ya Sergey Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia hapa mjini Tehran inapaswa kutathminiwa pia katika mtazamo wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

JCPOA ni makubaliano ya pande kadhaa yenye uungaji mkono wa kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hatima ya makubaliano haya hivi sasa limegeuka na kuwa suala la hadhi na heshima katika uga wa kimataifa. Hatua ya Marekani ya kukiuka makubaliano hayo imetoa pigo kubwa kwa heshima na hadhi ya kisiasa kimataifa kwa nchi nyingine zilizotia saini makubaliano hayo yaani Russia, China na madola matatu ya Ulaya.

Mazungumzo ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Sergey Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia

 

Wakati wa kukaribia kufanya safari hapa Tehran Lavrov alinukuliwa akisema kuwa, Russia imefikia natija hii kwamba, hakuna chaguo jingine mbadala ambalo linangilika akilini tofauti na Makubaliano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Katika mazingira kama haya, safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia hapa mjini Tehran inapaswa kutathminiwa kuwa ina umuhimu  na yenye malengo makubwa hasa kwa kuzingatia maudhui mbalimbali za pande mbili na pande kadhaa na katika fremu ya matukio yanayotokea hivi sasa katika eneo na vilevile mazingira maalum yanayotawala baada ya kusambaa virusi vya corona ulimwenguni.