Apr 13, 2021 11:38 UTC
  • Zarif: Ulaya haina hadhi wala nafasi ya kuwawekea vikwazo viongozi wa Iran

Akijibu hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuwawekea vikwazo viongozi na taasisi kadhaa za Iran Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: Ulaya haina hadhi wala nafasi ya kuwawekea vikwazo viongozi wa Kiirani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Russia, Muhammad Javad Zarif amesema kuwa, Ulaya inapasa kujirudi katika madai yake matupu na yasiyo na msingi eti ya kuheshimu haki za binadamu na badala yake izingatie uhakika wa mambo. Zarif amesema kuwa, nchi za Ulaya zinapasa kufikiria kuhusu hadhi na heshima yao. Ameongeza kuwa Ulaya haiko katika nafasi nzuri ya maadili na hivyo haifai kuuhubiria ulimwengu kuhusu suala hilo". 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Vitendo vya chuki dhidi ya wageni na dhidi ya Uislamu huko Ulaya vimeisababishia hali ya kutisha jamii ya Waislamu katika nchi hizo. Amesema kuwa nchi hizo hazina hadhi wala nafasi ya kuwawekea vikwazo viongozi wa Iran. 

Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia kwamba Iran haina tatizo lolote na kurejea katika kutekeleza majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA, na kwamba viongozi wa Marekani wanapasa kufahamu kuwa si vikwazo wala hatua za uharibifu  zitawafanya waweze kufanikisha mazungumzo; bali hatua hizo zinaifanya hali ya mambo kuwa tata zaidi kwao.  

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amevitaja vikwazo vya karibuni vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran kuwa ni kosa kubwa na vibaya zaidi kuliko uhalifu na kueleza kuwa, mwenendo huu wa Umoja wa Ulaya unaonyesha kuwa nchi hizo hazijui ni yapi yanajiri huko Ulaya kuhusu haki za binadamu. Lavrov  amesisitiza pia kuwa, jamii ya kimataifa inalaani jitihada zozote za kuvuruga mchakato wa JCPOA. 

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia