Apr 14, 2021 12:48 UTC
  • Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran; kwenda sambamba na Washington na Tel Aviv

Baraza la Umoja wa Ulaya Jumatatu tarehe 12 mwezi huu wa Aprili liliwajumuisha maafisa 8 na taasisi 3 katika ordha ya vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio cha eti kukiuka haki za binadamu. Aidha baraza hilo limechukua uamuzi wa kurefusha hatua zake dhidi ya Iran hadi tarehe 13 mwezi Aprili mwaka kesho kwa kisingizio cha kile ilichokitaja kuwa ukiukaji wa haki za binzdamu.

Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na makamanda wengine kadhaa wa ngazii ya juu wa jeshi hilo na Polisi ni miongoni mwa shakhsia wa Iran waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa kisingizio cha kukiuka haki za binadamu. Taasisi 3 pia yaani magereza ya  Evin, Fashafoyeh na Rajai Shahr yamewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.  

Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, vikwazo hizo vinajumuisha marufuku ya kuingia katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kuzuia fedha za maafisa hao waliowekewa vikwazo. Hatua hii ilianza kutekelezwa kwa mara ya kwanza mwaka 2011 na kila mwaka huongezwa muda kwa kutumia visingizio mbalimbali vya nchi za Ulaya. Hivi sasa na kwa kuzingatia vikwazo hivyo vipya, maafisa 89 na taasisi 4 za Kiirani zimewekwa kwenye faharasa ya vikwazo ya Umoja wa Ulaya. 

Inaonekana kuwa kitendo cha Umoja wa Ulaya cha kuiwekea Iran vikwazo hivi sasa kimetekelezwa katika fremu ya siasa zinazofanana za nchi za Magharibi mkabala wa Iran. Baada ya kuingia madarakani Rais mpya wa Marekani, Joe Biden, mwezi Januari mwaka huu, na sisiitizo la kiongozi la kuanzishwa tena uhusiano baina ya pande mbili za Bahari ya Atlantic (Trans- Atlantic), nchi za Ulaya zimefanya jitihada za kuchukua maamuzi yanayofafana na yale ya Washington kuhusu Iran na masuala yanayoihusu nchi hii kama mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kupinga uwezo wa makombora wa Iran na siasa za Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia.  

Umoja wa Ulaya na Troika ya umoja huo pia katika miezi mitatu ya hivi karibuni zilifanya juhudi za kutaka kuwa polisi mzuri na mbaya kwa wakati mmoja. Kwa upande mmoja zinadai kuwa zinataka kuyalinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA, na katika upande mwingine zinatoa vitisho na kutekeleza siasa za kupenda makuu.  

Catherine Ashton mkuuu wa zamani wa sera za nje za Umoja wa Ulaya anasema: "Biden anapasa kuyafanya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuwa makubaliano ya kwanza na si ya mwisho. Kamwe haikupangwa kwamba mapatano hayo yaliyofikiwa mwaka 2015 yawe nukta ya mwisho ya mazungumzo." 

Catherine Ashton, Mkuu wa zamani wa Sera za Nje wa EU 

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinazounda kundi la 4+1 ambalo linafungamanisha misimamo yake na serikali ya Biden, zilitoa pendekezo la kufanyika kikao kisicho rasmi kati ya wanachama wa JCPOA na Marekani kufuatia takwa la Washington la kutaka kuilazimisha Tehran ikubali masharti ya Washington;  jambo ambalo limepingwa vikali na Iran. 

Wakati huo huo vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran vimetangazwa wakati huu mazungumzo kuhusu mapatano ya JCPOA yakiwa katika hali nyeti. Pande husika ndani ya mapatano hayo zimekubaliana kwamba, vikao vya Kamisheni ya Pamoja ya mapatano hayo ya nyuklia katika ngazi ya manaibu mawaziri wa mambo ya nje vifanyike Jumatano ijayo huko Vienna na viendelee kufanyika katika fremu ya makundi ya wataalamu, mashauriano ya kiufundi na kwa upana zaidi ili kuweza kutayarisha na kuwasilisha orodha ya hatua zinazopasa kuchukuliwa na pande zote katika kuondoa vikwazo na hatimaye kuhisha mapatano hayo.  

Hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kufanya uharibifu katika taasisi ya nyuklia ya Natanz yaani kuzima mfumo wa kusambaza umeme ndani ya kituo hicho kwa leng la kusababisha madhara kwenye mashinepewa zinazofanya kazi katika taasisi hiyo, hujuma iliyokwenda sambamba na safari ya Loyd Aston Waziri wa Ulinzi wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) na misimamo aliyodhihirisha dhidi ya Iran Jumapili iliyopita, na wakati huo huo Umoja wa Ulaya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran siku ya Jumatatu, yote hayo yanaweka wazi mpango wa pamoja wa pande hizo. 

Hatua zote hizi ambazo zimekwenda sambamba na wakati mmoja na vilevile kuzidishwa mashinikizo ya kisiasa na vita vya kisaikolojia vya Washington dhidi ya Tehran ili ikubali matakwa ya Marekani juu ya namna nchi hiyo itakavyorejea katika mapatano ya JCPOA, zinaonyesha mpango wa pamoja ulioratibiwa na Brussels, Washington na Tel Aviv ili kuzidisha mashinikizo kwa Iran na kuvunja nguvu za Tehran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  Muhammad Javad Zarif amejibu mlolongo wa matukio yote haya akisistiza kuwa, viongozi wa Marekani wanapasa kuelewa kuwa si vikwazo wala hatua za uharibifu vinaweza kutumiwa kama wenzo wa mazungumzo, bali hatua zao hizi zitaifanya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi kwao. 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  

 

Tags