Apr 14, 2021 17:11 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Sera za Iran kuhusu JCPOA ziko wazi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumza kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na vikwazo na kusema sera za Iran ziko wazi kuhusu JCPOA na vikwazo. Ameongeza kuwa sera hizo amezibainisha wazi kwa wakuu wa nchi kupitia maandishi na katika mikutano.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatano jioni  mjini Tehran wakati akiwahutubia kwa njia ya video washiriki wa mahafali ya kuwa na ukuruba na Qur'ani Tukufu iliyofanyika katika siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini (MA). 

Kiongozi Muadhamu amesema, wakuu wa nchi wameamua kuenda kufanya mazungumzo ili sera hizo zitekelezwe na kuongeza kuwa ingawa hapingi suala hilo lakini kuna ulazima wa kuchukua tahadhari ili kuhakikisha kuwa mazungumzo  hayo hayaendelei kwa muda mrefu sana kwani hilo litakuwa kwa madhara ya nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, lengo la Wamarekani katika kusisitiza kuhusu mazungumzo ni kutaka kulazimisha kauli batili na kuongeza kuwa: "Mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, awali kabisa Marekani inapaswa kuondoa vikwazo kwani (Wamarekani) hawaaminiki. Huko nyuma walikiuka ahadi zao mara kadhaa kiasi kwamba  hata baadhi ya washiriki katika mazungumzo kutoka Ulaya wanakiri hilo katika vikao vya faragha ingawa wakati wa kuchukua maamuzi wanajisalimisha kwa Wamarekani na hawawezi kuchukua maamuzi huru."

Kingozi Muadhamu akisikliza qiraa ya Qur'ani Tukufu katika mahafali ya kuwa na ukuruba na Qur'ani Tukufu

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa,  aghalabu ya mapendekezo ya Wamarekani yamejaa kiburi na ni ya udhalilishaji kiasi kwamba hayawezi kutazmwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea matumaini yake kuwa, wakuu wa serikali nchini Iran watasonga mbele wakiwa waangalifu, kwa ukakamavu na kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba kwa taufiki na uwezo wake Mwenyezi Mungu wataweza kulifurahisha taifa.

Tags