Apr 15, 2021 02:25 UTC
  • Kimya cha IAEA baada ya uharibifu uliofanywa katika taasisi ya nyuklia ya Iran

Hujuma ya uharibifu iliyofanywa na Israel katika taasisi ya nishati ya nyuklia ya Natanz nchini Iran siku ya Jumapili iliyopita, kwa mara nyingine tena imeleta udharura wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kama taasisi kuu zaidi ya kimataifa inayosimamia shughuli za nyuklia dunia, kutoa jibu na kueleza wazi msimamo wake.

Taasisi ya nyuklia ya Natanz ni moja kati ya taasisi kadhaa za kurutubisha madini ya urani nchini Iran zinazosimamiwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimetangaza kuwa, uharibifu uliofanyika katika mtandao wa kusambaza umeme katika taasisi ya Natanz ni matokeo ya hujuma ya Israel na vimedai kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya vita ya utawala huo haramu dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran. Mwandishi wa gazeti la New York Times la Marekani, Ronen Bergman anasema: "Iwapo kutafikiwa mapatano mapya ya nyuklia, Israel itaendeleza vita vyake vya siri ili mapatano hayo yasitekelezwe kivitendo; na hili ndilo jambo linalofanyika hivi sasa. Hivi ni vita vya siri vya Israel ili kuhakikisha kwamba, miradi ya nyuklia ya Iran inafeli."

Baada ya hujuma hiyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiashiria vitisho vya hapo kabla vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran na kusema: "Shambulizi la makusudi dhidi ya taasisi ya nyuklia inayosimamiwa na wakala wa IAEA, sambamba na uwezekano mkubwa wa kuvujisha mada za radioactive, ni jinai na ugaidi wa kinyuklia."

Muhammad Javad Zarif

Kati ya nchi zote zenye miradi ya nyuklia duniani, Iran ndiyo iliyotishiwa mara kadhaa kushambuliwa taasisi na vituo vyake vya nyuklia. Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unamiliki silaha za nyuklia, daima umekuwa akisisitiza kuwa, utakabiliana na uwezo wa Iran katika teknolojia ya nyuklia.

Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi ameashiria shambulizi la Jumapili iliyopita dhidi ya taasisi ya nyuklia ya Natanz nchini Iran na kutilia mkazo udharura wa jamii ya kimataifa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia kukabiliana na ugaidi wa kinyuklia. Mbali na njama zake za mara kwa mara za kuwaua kigaidi wasomi na wataalamu wa masuala ya nyuklia wa Iran, ya hivi karibuni zaidi yakiwa mauaji ya mwaka jana 2020 ya

Mohsen Fakhrizadeh, aliyekuwa mtaalamu wa nyuklia na masuala ya ulinzi wa Iran, utawala haramu wa Israel katika miaka ya karibuni umekuwa ikipanga na kutekeleza hujuma za kimtandao na za kawaida dhidi ya taasisi za nyuklia nchini Iran.


Mohsen Fakhrizadeh

Moja kati ya mashambulizi hayo ya kimtandao ni lile lililofanywa na Israel ikishirikiana na Marekani dhidi ya kituo cha Natanz kwa kutumia virusi vya Stuxnet. Mwaka mmoja baada ya hujuma hiyo ya kimtandao, yaani Julai mwaka uliopita wa 2020, kulitokea mlipuko katika ukumbi wa kuzalisha mashinepewa huko Natanz ambapo vyombo vya habari na hata wataalamu wa Israel walikiri kwamba wamehusika na hujuma hiyo. Wakati huo balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika jumuiya za kimataifa mjini Vienna  alihutubia kikao cha Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kutangaza kuwa mlipuko huo ni matokeo ya kitendo cha uharibifu na akautaka wakala huo na wanachama wake kukilaani vikali. Hata hivyo wakala wa IAEA na Mkurugeni Mkuu wake, Rafael Grossi, ulijiepusha kulaani hujuma hiyo ya kigaidi. Hii ni licha ya kwamba, maazimio mbalimbali ya wakala wa IAEA yanasisitiza kuwa, hujuma yoyote ya silaha au vitisho dhidi ya taasisi ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ambayo inakaguliwa na wakala huo ni ukiukaji wa hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Rafael Grossi

Sasa na baada ya uharibifu mwingine uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika taasisi ya nyuklia ya Natanz ambao umesababisha madhara kwenye mfumo wa kusambaza umeme wa taasisi hiyo kama matokeo ya mlipuko, kunajitokeza swali kwamba, ni kwa nini Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia na Mkurugenzi Mkuu wake wanajiepusha kuchukua msimamo kuhusu kadhia hii? Hii ni licha ya kwamba, wakala huo unaelewa vyema kwamba, hujuma hiyo inakiuka sheria za kimataifa na manuni za wakala huo wenyewe.

Haya yote yanaonyesha kuwa, kinyume na madai ya Rafael Grossi kwamba, wakala huo haupendelei upande wowote, chombo hicho na viongozi wake wamenyamazia kimya hujuma na vitendo hivyo vya Israel vinavyokiuka sheria za kimataifa.          

Tags