Apr 15, 2021 03:13 UTC
  • Rouhani: Urutubishaji urani hadi asilimia 60 ni jibu kwa shari

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa urutubishaji wa madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 60 ni jibu kwa vitendo vya shari vya maadui.

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri ambapo amesema hatua ya Iran ya kuanza kutumia mashinepewa au sentrifuji za kisasa aina ya IR-6 na urutubishaji wa madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 60 ni jibu muafaka kwa vitendo vya shari vya maadui. Ameongeza kuwa, iwapo Wazayuni watatekeleza njama dhidi ya Iran, basi tutatoa jibu na hilo ndilo jibu la kwanza.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, hilo ni jibu kwa ukhabiti wa Wazayuni ili wafahamu kuwa hawawezi kupanga njama dhidi ya taifa la Iran na kutenda jinai katika kituo cha nyuklia cha Natanz.

Mashinepewa aina ya IR-6

Rais wa Iran alikuwa akishiria tukio la hivi karibuni la uharibifu uliofanywa katika kituo cha nyuklia cha Natanz katikati mwa Iran siku chache zilizopita. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipiza kisasi kwa wakati mwafaka kutokana na uharibifu uliofanywa na Israel katika kituo hicho cha Natanz.

Kwingineko Rais Rouhani ameongeza kuwa: "Tutakata mikono ya Wazayuni wanapotenda jinai." Aidha amesema Iran itashinda katika vita vya kiuchumi na hatimaye dhulma itafika ukingoni.

Hali kadhalika Rais wa  Iran ameendelea kusema kuwa, wale ambao wameyachukua mateka maisha ya watu na kutatiza jitihada za Iran za kupata chanjo na vyakula wafahamu kuwa lazima mikono yao itakatwa.

Rais Rouhani ametoa shukrani zake za dhati kwa sekta ya afya nchini Iran na kusema sekta hiyo ina jukumu zito sana wakati huu wa janga la corona.

Kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, Rais Rouhani amesema Marekani lazima irejee katika mapatano hayo kama ilivyokuwa wakati yalipofikiwa mwaka 2015. Amesema Iran imetangaza bayana kuwa pale Marekani itakapochukua hatua za kivitendo za kutekeleza ahadi zake, Iran nayo itarejea katika kutekeleza ahadi zake za mapatano ya JCPOA.