Apr 16, 2021 03:35 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu mazungumzo ya nyuklia; sharti la Iran, msingi wa kuhuishwa JCPOA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, siasa za Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ziko wazi, na maafisa wanaoshiriki kwenye mazungumzo ya kuhuishwa makubaliano hayo wanapaswa kuwa macho ili yasirefushwe kupita kiasi, suala ambalo lina madhara kwa taifa.

Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo Jumatano wiki hii katika majlisi ya kisomo cha Qur'ani. Akizungumzia masuala yanayohusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, vikwazo na mazungumzo yanayoendelea huko Vienna, Ayatullah Khamenei amesema, lengo la Wamarekani wanaposisitiza na kung'ang'ania mazungumzo, ni kutaka kuutwisha upande wa pili matakwa yao haramu. 

Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 4+1 ilianza siku kumi zilizopita huko Vienna kwa shabaha ya kuhuisha makubaliano ya JCPOA na kufutwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, baada ya Tehran kujihakikishia kwamba, vikwazo hivyo vimefutwa kivitndo. Mantiki ya Iran katika mazungumzo ya sasa ni kwamba, katika hatua ya kwanza Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyake dhidi ya Iran, kwa sababu tajiriba na uzoefu vimeonyesha kuwa, Marekani haiaminiki na ilikiuka na kukanyaga majukumu ya kwa kujiondoa katika makubaliano hayo kinyume cha sheria. 

Mazungumzo ya nyuklia ya Vienna

Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo ya nyuklia, nchi za Ulaya nazo hazikutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA na kivitendo ziliungana na serikali ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump. Japokuwa nchi hizo za Ulaya wanachama katika makubaliano ya JCPOA zilikiri kwamba, Marekani imekiuka na kukengeuka majukumu yake, lakini zilisalimu amri mele ya serikali ya Washington na kama aliyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, hazijitawali wala kuwa huru katika kuchukua maamuzi.

Baada ya kushika madaraka serikali ya Joe Biden huko Marekani, zilianza jitihada za kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kupitia mazungumzo na harakati za kidiplomasia, na hatimaye kukaanzishwa mazungumzo ya Vienna. 

Sera kuu ya Iran katika jitihada za kuhuisha makubaliano ya JCPOA ni kufutwa, kivitendo, vikwazo dhalimu vya Marekani, na Tehran haitakubali mpango au pendekezo lingile lolote ghairi ya msimamo huo. Inasikitisha kuona kwamba, mwenendo wa serikali ya Joe Biden kuhusiana na JCPOA ni ule ule wa mtangulizi wake, yaani Donald Trump, kwa sababu hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ametahadharisha kuhusu ujanja na mbinu ya Wamagharibi ya kutaka kurefesha kupita kiasi mazungumzo hayo na kuuchosha upande wa Iran. 

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mahmoud Vaezi alisema Jumatano wiki hii kwamba: "Kadiri mazungumzo hayo yanavyorefushwa ndivyo mashinikizo ya vikwazo yanavyozidi kwa taifa la Iran. Hii ni licha ya kwamba, serikali mpya ya Marekani ilitangaza kuwa, siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu za serikali ya Washington zimefeli lakini kivitendo inaendeleza vikwazo hivyo na kufuata nyayo za serikali ya Trump."

Vaezi

Kufeli kwa siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kumethibitisha kuwa, mashinikizo, vitisho na uharibifu haviwezi kuilazimisha Iran isalimu amri kwenye meza ya mazungumzo, na njia pekee ya kuhuishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kufutwa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya taifa la Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya nyuklia na kuanza operesheni ya kuzalisha madini ya urani iliyorutubishwa kwa asilimia 60 katika taasisi ya nyuklia ya Natanz, likiwa jubu la ugaidi wa kinyuklia na uhaibifu uliofanywa na maadui katika kituo hicho, kumeonyesha kwamba Iran haiwezi kutishwa na itaendelea na miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Kama alivyosema Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif, ugaidi hatari wa kinyuklia huko Natanz utakomeshwa kwa kusitishwa ugaidi wa kiuchumi wa serikali ya Donald Trump. Kwa msingi huo serikali ya Joe Biden huko Marekani inaweza tu kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutupilia mbali vikwazo dhidi ya Iran na kutekeleza majuku yake; la sivyo fursa ya sasa ya mazungumzo ya Vienna itayoyoma kama mawimbi.       

Tags