Apr 17, 2021 02:44 UTC
  • Iran yajibu matamshi ya kuingilia masuala yake ya ndani yaliyotolewa na Arab League na GCC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameiasa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (P) GCC badala ya kuungana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kutoa tuhuma kila mara dhidi ya Iran zielekeze macho yao kwa shughuli za kijeshi za nyuklia na zilizo kinyume na sheria zinazofanywa na utawala huo.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo kujibu matamshi ya uingiliaji masuala yake ya ndani yaliyotolewa na taasisi ziitwazo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi, ambapo sambamba na kuzikumbusha nafasi haribifu ya baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hizo amesisitiza kuwa, matamshi hayo ya kiuanagenzi na yasiyo ya uwajibikaji ni mwendelezo wa kauli zinazotolewa dhidi ya Iran, ambazo lengo lake si kuomba kushirikishawa, bali ni kutaka kuvuruga mchakato wa mazungumzo ya kiufundi yanayoendelea mjini Vienna.

Khatibzadeh ameongeza kuwa, makatibu wakuu wa taasisi hizo mbili wajue kwamba, Iran ni mwanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki; na shughuli zote za nyuklia za jamhuri ya Kiislamu zinafanyika chini ya uangalizi wa wakala huo, hivyo ni wazi kwamba ustawishaji au upanuzi wa shughuli hizo utaendelea kufanyika kulingana na haki zinazotambulika kisheria za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa na kwa madhumuini ya kudhamini mahitaji ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Nayef bin Falah Mubarak Al-Hajraf

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amewataka makatibu wakuu wa jumuiya hizo za Kiarabu wafikirie zaidi hatari ya vichwa vya nyuklia vinavyomilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao kutokana na kutokuwa mwanachama wa mkataba wa NPT, unaopiga marufuku uundaji silaha za nyuklia, ndio tishio kubwa zaidi la amani na uthabiti katika eneo hili.

Siku ya Jumatano, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (P) GCC Nayef bin Falah Mubarak Al-Hajraf alidai kuw,a kuna udharura wa nchi wanachama wa baraza hilo kushirikishwa katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA; na katika barua aliyowaandikia mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani alidai kwamba GCC ndiyo yenye mchango mkuu wa kuimarisha amani na uthabiti katika eneo hili.

Mubarak al-Hajraf alidai pia kwamba, mazungumzo ya sasa ya Vienna yasihusishe mpango wa nyuklia tu wa Iran, bali yajumuishe pia mienendo ya Iran aliyodai kwamba inavuruga uthabiti katika eneo pamoja na makombora ya balestiki na ndege zake zisizo na rubani.../

Tags