Apr 17, 2021 12:34 UTC
  • Picha ya aliyefanya uharibifu katika kituo cha nyuklia cha Iran, yasambazwa + Video

Wizara ya Masuala ya Kijasusi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesambaza picha ya aliyefanya uharibifu katika kituo cha nyuklia cha Natanz hivi karibuni humu nchini.

Mashirika mbalimbali ya habari ya Iran yametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Masuala ya Kijasusi humu nchini imefanikiwa kumgundua aliyefanya uharibifu katika kituo hicho cha nyuklia na kusambaza picha yake kwa mara ya kwanza kabisa.

Reza Karimi (43) ndiye muhusika mkuu wa uharibifu huo na alitoroka nchi kabla ya kutokea tukio hilo. Hata hivyo tayari Iran imeshachukua hatua za kisheria za kuhakikisha anarejeshwa humu nchini.

Jumapili ya wiki iliyopita, sehemu moja ya umeme ya taasisi ya urutubishaji urani ya Shahid Ahmadi Roushan katika kituo cha nyuklia cha Natanz ilikumbwa na tatizo nchini Iran.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulijigamba kuwa ndio uliofanya uharibifu huo huku vyombo vya habari vya Magharibi vikilivalia njuga mno suala hilo mpaka kufikia kudai kuwa eti urutubishaji urani nchini Iran utasimama kwa miezi kadhaa kutokana na uharibifu huo.

Hata hivyo kazi ya urutubishaji urani kwa asilimia 60 inaendelea katika kituo hicho na matunda yake yameanza kutolewa.

Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesisitiza kuwa, uharibifu huo haukuathiri zoezi hilo na urani iliyorutubishwa kwa asilimia 60 tayari imeanza kuzalishwa.