Apr 22, 2021 03:58 UTC
  • Rouhani: Taifa la Iran linajivunia vikosi vyake vya ulinzi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Artesh) na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ni vikosi vya ulinzi ambavyo daima vimekuwa katika medani. Ameongeza kuwa, taifa la Iran linajivunia jitihada na kujitolea muhanga kwa vikosi hivyo vya ulinzi katika kipindi cha miaka 42 iliyopita.

Rais Rouhani aliyasema hayo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri na huku akiashiria Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kislamu ya Iran iliyoadhimishwa hivi karibuni amesema: "Tarehe 18 Aprili 1979, kwa amri ya Imam Khomeini MA, ilitangazwa kuwa Siku ya Jeshi. Hii ni siku ambayo kote Iran, wananchi walishiriki katika maandamano makubwa na kupiga nara ya  "Taifa Linajitolea Kwa Jeshi" nao wanajeshi wakajibu kwa kusema , "Jeshi Linajitolea kwa Taifa", na kwa njia hiyo njama kubwa ambayo ilikuwa imepangwa ya kulivunja jeshi ikasamabratishwa .

Rais wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa: "Siku chache baada ya tukio hilo, Imam Khomeini MA alitangaza kuasisiwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu." Amesema Dikri zote mbili hizo zilikuwa muhimu kwani iwapo Imam MA hangechukua hatua ya kuhuisha jeshi na kisha kuasisi IRGC katika wakati huo basi kungejiri maafa makubwa katika historia kutokana na vita vya kulazimishwa.

Rais Rouhani ameashiria kadhia ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: "Sisi tunataka mapatano ya JCPOA yatekelezwe kama ilivyoanishwa, utekelezwaji huo usizidi wala kupungua hata neno moja. Sisi hatujitakii makuu lakini tuna matakwa ambayo tutayataja baadaye. Katika miaka minne iliyopita tumepata hasara ya mamia ya mabilioni ya dola. Kile ambacho sasa kinatakiwa ni kutekelezwa mapatano ya JCPOA bila kuongezwa au kupunguzwa."

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa, Wamarekani wanapaswa kuondoa vikwazo vyote  dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: "Sisi ndio tutakaoainisha iwapo vikwazo vimeondolewa au la na tutakapopata hakikisho basi tutatangaza kuwa vikwazo vimeondolewa."

 

Tags