Apr 23, 2021 02:41 UTC
  • Kamanda Fallahzadeh: Vikosi vya muqawama vipo karibu na kambi za Israel kote duniani

Naibu Kamanda mpya wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ametahadharisha kuwa, vikosi vya muqawama vipo karibu sana na kambi za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel katika pembe mbalimbali za dunia.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Fallahzadeh alitoa onyo hilo jana Alkhamisi mjini Isfahan katikati mwa Iran katika kikao cha kumuenzi na kumuomboleza mtangulizi wake, Sayyid Mohammad Hosseinzadeh Hijazi.

Brigedia Jenerali Fallahzadeh ameeleza bayana kuwa, makundi ya muqawama yanausukuma utawala haramu wa Israel kwenye ncha ya kuporomoka katika kila dakika.

Huku akiapa kufuata nyayo za mtangulizi wake, Naibu Kamanda mpya wa Kikosi cha Quds cha SEPAH amekariri kauli iliyowahi kutolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kwamba, utawala wa Kizayuni hautakuwepo hai katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Wanamuqawama wanaoutia kiwewe utawala wa Kizayuni

Amesema damu za Mashahidi (Qassem) Soleimani na Hijazi zinapita katika mishipa ya umma wa Kiislamu na haziwezi kupotea hivi hivi; na kwamba mataifa ya Kiislamu yataendeleza mapambano hadi pale bendera ya Uislamu itakapopepea katika kila kona ya dunia.

Naibu Kamanda mpya wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amerithi mikoba ya Brigedia Jenerali Mohammad Hosseinzadeh Hijazi, ambaye aliaga dunia Jumapili iliyopita akiwa na umri wa miaka 65, kutokana na mshtuko wa moyo.

Tags