Apr 30, 2021 03:12 UTC
  • Imarati yaunga mkono msimamo mpya wa Saudia kuhusu Iran

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ameelezea kufurahishwa kwake na msimamo mpya wa Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kuhusu kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Middle East News iliripoti jana (Alkhamisi) kwamba, Mohammed bin Zayed Aal Nahyan, mrithi wa kiti cha ufalme wa Abudhabi ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, mahojiano ya televisheni aliyofanya Bin Salman ni mazuri na kwamba kuchukuliwa msimamo huo mpya wa Saudia kuhusu Iran ni hatua nzuri na muhimu kwa nchi za eneo hili na dunia nzima kiujumla. 

Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia alisema katika mahojiano aliyofanyiwa juzi Jumatano na televisheni ya nchi hiyo ya al Arabia kwamba, Iran ni nchi jirani; na Riyadh ina matumaini kwamba itaweza kuwa na uhusiano mzuri na Tehran.

Bin Salman katika mahojiano ya hivi karibuni na televisheni ya nchi hiyo ya al Arabia. Alidai anataka uhusiano mzuri na Iran

 

Mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia alieleza pia kwamba, utawala wa Riyadh unashauriana na nchi za kanda na za ulimwengu kwa ujumla ili kutafuta njia ya kuwezesha kuwa na uhusiano mzuri na Iran kwa manufaa ya wote.

Aidha Bin Salman aliashiria malengo ya pamoja ya nchi mbili na akasema, Riyadh haitaki Iran iwe katika wakati mgumu, bali inataka iwe nchi iliyostawi; na matakwa hayo ni kwa ajili ya kulifanya eneo hili lote na nchi zote za dunia kupiga hatua kueleka kwenye ustawi na maendeleo.

Tags