Apr 30, 2021 03:17 UTC
  • Spray ya kwanza ya kupambana na corona ya Iran, yazinduliwa rasmi

Sherehe za kuzinduliwa rasmi spray ya kwanza ya kupambana na kirusi cha corona, ya Kiirani, zilifanyika jana Alkhamisi katika Hospitali ya Masih Daneshvari hapa jijini Tehran.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Iran Press ambalo limeongeza kuwa, Dk Ali Akbar Velayati, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Masih Daneshvari, Aliereza Zali, Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona mjini Tehran na Peyman Salehi, Makamu wa Rais wa Iran katika masuala ya teknolojia wameshiriki kwenye sherehe hizo.

Katika sherehe hizo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Masih Daneshvari, Daktari Velayati amesema, kutumia barakoa bado ndiyo njia bora zaidi ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. 

Amesema, kwa msaada wa Kitengo cha Sayansi na Teknolojia cha ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, karibuni hivi kutaanza kuzalishwa kwa wingi spray hiyo ya kukabiliana na kirusi cha corona.

Sherehe za uzinduzi wa spray ya kwanza ya Iran ya kupambana na COVID-19

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Corona mjini Tehran masisitiza kuwa, barakoa ndiyo njia bora zaidi ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 na kuongeza kwamba, kazi ya spray hiyo ya kupambana na corona iliyozinduliwa jana Alkhamisi hapa Tehran ni kukivunja nguvu mara moja kirusi cha corona wakati kinapotua juu ya barakoa au juu ya nguo.

Siku chache zilizopita pia, Mkurugenzi wa timu ya utafiti na uzalishaji wa chanjo ya COVIRAN BAREKAT Hassan Khalili alisema kuwa, uzalishaji wa chanjo hiyo ya corona ya Kiirani uko katika hatua zake za mwisho na kwamba itaanza kutolewa bure kwa watu wote humu nchini kuanzia mwezi ujao wa Khordad wa kalenda ya Hijria Shamsia.

Tags