May 07, 2021 08:21 UTC
  • Kurejea Wapalestina katika ardhi zao ndio suluhu ya kadhia ya Palestina

Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu limesema kutimuliwa Wazayuni maghasibu na kurejea Wapalestina katika ardhi za mababu zao ndilo suluhisho pekee la mgogoro wa Palestina-Israel.

Baraza hilo limesema hayo Alkhamisi katika taarifa yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds inayoadhimishwa leo Ijumaa kote duniani.

Taarifa hiyo imesema Siku ya Kimataifa ya Quds haiwahusu tu Wapalestina, bali ni siku inayouhusu Umma wote wa Kiislamu.

Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu limebainisha katika taarifa hiyo kuwa, hii leo dunia inashuhudia matunda ya muqawama na mapambano katika ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya utawala dhalimu na katili wa Israel.

Limesema linaamini kuwa Umma wa Kiislamu hatimaye utainusuru Palestina na uweze kurejesha umiliki na usimamizi wa Quds tukufu mikononi mwa Waislamu.

Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu limetoa taarifa hii wakati huu ambapo Waislamu na wapenda haki wanashiriki vikao na maandamano katika pembe mbalimbali za dunia katika Siku ya Kimataifa ya Quds.

Siku hii ni ya kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

 

Tags