May 08, 2021 09:18 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Mustakbali bora wa Palestina utapatikana kwa muqawama na uungaji mkono wa wote

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Wazayuni wanaoikalia kwa mabavu Palestina, wameigeuza nchi hiyo kuwa kambi ya kigaidi tangu siku kwanza kabisa ya kuanza kuikalia kwa mabavu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika hotuba ya kwenye televisheni aliyoitoa jana Ijumaa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds na kusisitiza kuwa, Israel si nchi bali ni kambi ya kigaidi dhidi ya taifa la Palestina na mataifa mengine ya Waislamu na kwamba kupambana na utawala huo katili ni kupambana na dhulma na ni kupambana na ugaidi, na hilo ni jukumu la kila mmoja wetu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kuna mambo mawili ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kupatikana mustakbali bora wa Palestina. Jambo la kwanza na ambalo ndilo muhimu zaidi ni kuendelea muqawama ndani ya ardhi za Palestina na kutiwa nguvu fikra ya jihadi na kufa shahidi. Jambo la pili ni uungaji mkono wa kimataifa, wa tawala na mataifa ya Waislamu kote dunia kwa wanajihadi wa Palestina.

Maandamano ya Waislamu Tanzania Siku ya Kimataifa ya Quds

Kadhia ya Palestina na Quds ni moja ya masuala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu na ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiunga mkono haki na malengo matukufu ya Palestina; kisiasa, kimaanawi na kimaada, katika mazingira yoyote yale.

Iran ambayo ndiye muungaji mkono mkuu wa haki za Wapalestina imetoa mchango mkubwa sana katika kipindi cha miongo minne iliyopita katika kulibakisha hai suala muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa yaani Palestina na Quds. Ubunifu wa Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds lilikuwa ni jiwe la msingi na fursa ya dhahabu ya kulibakisha hai suala hilo ambalo linauhusu umma wote wa Kiislamu.

Haider bin Ali al-Lawati, mhadhiri wa Chuo Kuu nchini Oman aliandika juzi Alkhamisi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Palestina si suala muhimu sana kwa Wapalestina na Waarabu tu, bali kadhia ya Palestina ni suala muhimu mno kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Maandamano makubwa ya Waislamu wa Yemen, Siku ya Kimataifa ya Quds

Mbali na uungaji mkono wa kisiasa na kimaanawi, kuungwa mkono kimaada muqawama wa Palestina pia ni jukumu la kila mmoja wetu katika umma na nchi za Kiislamu kutokana na kwamba utawala wa Kizayuni umejengeka juu ya msingi wa kigaidi. Muqawama na kuimarishwa makundi ya Palestina ndilo chaguo pekee la kiistratijia na lenye manufaa katika kupambana na Israel hasa kwa kuzingatia kuwa utawala huo ghasibu daima umekuwa ukiendesha vitendo vya kigaidi ndani na nje ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Kuuawa shahidi na kujeruhiwa kila siku wananchi na hasa vijana wa Palestina kunakofanywa na wanajeshi makatili wa Israel na vilevile njama za kila namna za Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi ikiwemo njama kubwa ya "Muamala wa Karne" zote hizo zimeshindwa kukabiliana na kuuvunja nguvu muqawama wa Wapalestina na ni kwa sababu hiyo ndio maana leo hii Israel inapitisha kipindi kigumu zaidi na dhaifu zaidi katika historia yake yote.

Matukio ya hivi karibuni, likiwemo shambulio la kombora karibu na taasisi za nyuklia za Dimona za Israel, kushambuliwa maeneo kadhaa nyeti mno ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kusimama imara vijana wa Palestina katika kukabiliana na wanajeshi makatili wa Israel kwenye Msikiti wa al Aqsa, kumebadilisha mlingano wa kisiasa na kijeshi kwa manufaa ya vijana wa Palesitna. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana tukasema kuwa, uungaji mkono wa pande zote wa serikali na mataifa ya Waislamu kwa taifa madhulumu la Palestina ni jukumu la kila mmoja wetu katika Umma mzima wa Kiislamu.

Tags