May 09, 2021 12:45 UTC
  • Spika Qalibaf: Tunachofuatilia ni vikwazo vyote kuondolewa kikamilifu

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran inataka vikwazo vyote viondolewe kikamilifu.

Mohammad Baqir Qalibaf ameyasema hayo leo katika kikao cha wazi cha bunge na kubainisha kwamba, tunafuatilia vikwazo vyote kuondolewa kikamilifu, kivitendo na kwa haraka sana kulingana na sera zilizoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Qalibaf ameongeza kuwa, ikiwa vikwazo vyote vitaondolewa kikamilifu na athari zake za kiuchumi zikathibitika kivitendo, haitapasa kuchelewesha hata kwa saa moja kutekeleza majukumu ambayo Iran imeyakubali kulingana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Spika wa Bunge la Iran aidha amesema, maadui wa Iran wajue kwamba wananchi wa Iran hawatokaa katu kungojea hatua zao, licha ya kufanya jitihada za kuondolewa vikwazo.

Dakta Qalibaf amekumbusha pia kuwa, Iran ndiyo iliyokamata mpini wa uchukuaji hatua na akasema: badala ya maadui kuzidi kuwa na uchu wa kujivutia upande wao na kusuasua katika mazungumzo, watekeleze kikamilifu na kivitendo majukumu yao na kutopoteza muda zaidi katika kuondoa vikwazo, kwa sababu kadiri muda unavyopita, ndivyo itakavyowagharimu zaidi kurudi kwenye makubaliano ya JCPOA.

Spika wa Majlisi ya ushauri ya Kiislamu ya Iran ameitaka pia timu ya ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna iendelee kuchukua misimamo kwa kufuata na kushikamana na sera zilizoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.../  

Tags