May 10, 2021 07:49 UTC
  • Mustafa al-Kadhimi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiunga mkono serikali ya Iraq

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, Wairani ni watu wa kutazama mambo kwa uhalisia wake na kwamba, juhudi zao zinalenga kuiunga mkono serikali ya Baghdad na wala hazina nia ya kuidhoofisha.

Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi amesisitiza kuwa, daima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiiunga mkono serikali ya Iraq na kufanya juhudi za kukabiliana na njama za wanamgambo na makundi ya waasi zinazolenga kuidhoofisha serikali ya Baghdad.

Huko nyuma pia Mustafa al-Kadhimi amewahi kunukuliwa mara chungu nzima akisema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mshirika wa kistratejia wa Iraq na kuthamini na kusifu mchango, himaya na uungaji mkono wa Tehran katika vita  dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq akiwa katika mazungumzo na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya safari zake jijini Tehran (Picha kutoka maktaba)

 

Aidha al-Kadhimi amelaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na hatua yayke ya kuwazuia Waislamu kwenda katika maeneo yao matakatifu na kusema kuwa, kwa mtazamo wa Baghdad ni kuwa, kama kuanzisha uhusiano wa kawaida (na utawala haramu wa Israel) hakupelekei kupatikana haki za taifa la Palestina, basi ni jambo ambalo katu halikubaliki.

Kadhalika Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa, kile kinachofanywa na utawala haramu wa Israel huko Palestinaa dhidi ya wananchi madhulumu tena katika ardhi zao hakikubaliki hata kidogo, hivyo kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka na za maana za kukabiliana na hatua na jinai hizo za Wazayuni maghasibu.

Tags