May 11, 2021 02:51 UTC
  • Iran yaanza kuwasajili wagombea wa uchaguzi wa rais leo

Usajili wa wagombea wa awamu ya 13 ya uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeanza leo Jumanne.

Usajili huo unaofanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi umeanza saa mbili asubuhi kwa saa za hapa nchini, na unatazamiwa kuendelea hadi Mei 15.

Baada ya kumalizika uandikishaji huo unaofanyika kwa muda wa siku tano, majina ya wagombea wenye azma ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwezi ujao yatakabidhiwa Baraza la Katiba.

Baraza hilo lenye wanachama 12 litatathmini na kuyapiga msasa majina hayo, na kuwapasisha watakaokuwa wamekidhi vigezo na masharti ya kugombea urais hapa nchini.

Rais Hassan Rouhani wa Iran anayemaliza muda wake wa uongozi wa mihula miwili

Baraza hilo lina hadi Mei 25 kuwachuja wagombea watakaojitokeza, na linatazamiwa kutoa orodha ya mwisho ya wawaniaji wa uchaguzi wa urais hapa nchini kati ya Mei 26 na 27.

Wagombea watakaodhinishwa na Baraza la Katiba wanatarajiwa kuanza kampeni katika muda utakaoanishwa hapo baadaye, kuelekea uchaguzi wa rais uliratibiwa kufanyika Juni 18.

 

 

Tags