May 11, 2021 07:45 UTC
  • Wanachuo wakusanyika mjini Tehran kulaani jinai za Wazayuni Ukanda wa Ghaza

Kundi la wanafunzi wa Iran na wa kigeni wa Chuo Kikuu cha Tehran wamekusanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa Tehran, kulaani jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.

Katika mkusanyiko huo, wanachuo hao wamepiga nara za kuilaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutangaza hasira zao kwa jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizyauni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi, wakiitaka jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa kutokaa kimya mbele ya jinai hizo.

Wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha Tehran wamebeba bendera ya mita 20 ya Palestina ikiwa ni kutangaza umoja na mshikamano wao kwa taifa la Palestina.

Sehemu ya mkusanyiko wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran kuliunga mkono taifa la Palestina

 

Vile vile wanachuo wa Kiirani na wa kigeni wa chuo kikuu hicho maarufu kimataifa wametoa tamko wakisisitiza kuwa, taifa la Palestina linatambua vyema kwamba, kusimama kidete na muqawama ndiyo njia pekee ya kukabiliana na dhulma na kuweza kukomboa ardhi na haki zao zinazokanyagwa na Wazayuni.

Sehemu nyingine ya tamko hilo la pamoja la wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha Tehran imesema, leo hii mji mtukufu wa Baitul Muqaddas umekumbwa na jinai za kutisha za Wazayuni ambazo zinauhuzunisha na kuushitua kila moyo wa mwanadamu mwenye hisia za utu. Jinai hizo zimeongeza hasira za wanadamu huru dunia kutokana na uvamizi na ukatili wa kuchupa mipaka wa Wazayuni.

Vile vile taarifa hiyo imesema, dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel usingelishuhudiwa kama Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa zisingelikuwa zinanyamazia kimya jinai za Wazayuni.

Tags