May 11, 2021 07:50 UTC
  • Ghalibaf: Damu ya Shahid Soleimani imetoa msukumo wa mamia ya mara kwa muqawamaa

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, damu ya Shahid Qassem Soleimani imetoa msukumo wa mamia ya mara kwa muqawama katika kona mbalimbali za dunia.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, matukio ya mfululizo ya kulipiza kisasi dhidi ya jinai za Wazayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yanathibitisha kwamba usaliti wa kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni pamoja na damu ya shahid Soleimani ni mambo ambayo yameongeza kwa mamia ya mara hamasa na msukumo wa kusimama imara umma wa Kiislamu, kupambana na maghasibu.

Shahid Qassem Soleimani

 

Spika wa Bunge la Iran vile vile ameandika: Jinai ya Wazayuni maghasibu ya kuvamia maeneo matakatifu na kuwashambulia kikatili Waislamu waliokuwa wanasali, kuuvunja heshima Msikiti wa al Aqsa na kufanya ukatili mkubwa dhidi ya wakazi wa mji wa Quds pamoja na jinai za kinyama zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa eneo la Sheikh al Jarrah ni uthibitisho wa kuchanganyikiwa utawala wa Kizayuni unaoikalia Quds kwa mabavu.

Msikiti wa al Aqsa na maeneo ya pembeni mwake huko Baytul Muqaddas Palestina, kwa siku kadhaa sasa yamekumbwa na mashambulizi ya kikatili ya wanajeshi wa Israel wanaojaribu kukandamiza muqawama wa Wapalstina. Hadi sasa mamia kadhaa ya wakazi wa Quds tukufu wameshajeruhiwa na wengine wameshauawa.

Tags