May 11, 2021 11:48 UTC
  • Iran yazindua shehena ya kwanza kwa ajili ya matumizi rasmi, ya chanjo ya COV-Iran Barekat

Mkuu wa Tume ya Utekelezaji Maagizo ya Imam Khomeini (MA) amesema, dozi milioni 30 za chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 iliyotengenezwa na wataalamu wa Kiirani ya COV-Iran Barekat zitakuwa zikizalishwa kila mwezi hapa nchini.

Mohammad Mokhber ameyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa shehena ya kwanza ya chanjo ya corona aina ya COV-Iran Barekat iliyozalishwa kwa wingi kwa ajili ya matumizi rasmi.

Mkuu wa Tume ya Utekelezaji Maagizo ya Imam Khomeini (MA) ameongeza kuwa "leo Jumanne tumekabidhi dozi laki tatu za chanjo hii na hadi ifikapo mwezi Septemba tutakuwa tumefikia uwezo wa kukabidhi dozi milioni 30."

Chanjo ya Covid-19 ya COV-Iran Barekat

Kuhusu majaribio ya kitiba iliyofanyiwa chanjo ya COV-Iran Barekat hadi sasa, ambayo yamefanyika sambamba na awamu ya tatu ya majaribio ya chanjo hiyo, Mokhber amesema: matokeo ya majaribio hayo yalikuwa ya mafanikio kwa takriban asilimia 100 na kwamba matokeo ya awamu ya kwanza na ya pili yalikuwa na taathira chanya kwa asilimia 100, hivyo kuna matumaini kuwa taathira ya awamu ya tatu pia itakuwa ni ya asilimia 100.

Mbali na COV-Iran Barekat, wataalamu na wanasayansi wa Kiirani wamefanikiwa kutengeneza na kuzalisha aina nyingine kadhaa za chanjo ya kinga ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ambazo zimesifiwa katika duru za kielimu na kisayansi duniani.../