May 13, 2021 02:14 UTC
  • SEPAH: Tutaunga mkono kwa nguvu kubwa zaidi mapambano ya wananchi wa Palestina

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran SEPAH limetoa tamko rasmi na kusisitiza kuwa, hivi sasa na kuendelea litaunga mkono mapambano na intifadha ya taifa la Palestina kwa nguvu kubwa zaidi kuliko huko nyuma.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, katika tamko lake hilo, jeshi la SEPAH limelaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni katika Msikiti wa al Aqsa na kuwaua shahidi makumi ya Wapalestina wasio na hatia kwenye miji ya Quds na Ghaza na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel na kusisitiza kuwa, Intifadha ya Ramadhani na kuzidi kuwa mpana wigo wa muqawama kumefichua zaidi dhati ya kishetani ya Israel ghasibu na waungaji mkono wake makhabithi.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH aidha limesisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, majibu ya kutia moyo na ya kufurahisha ya wanajihadi na wanamapambano wa makundi ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina, yamewatumbukiza Wazayuni katika mgogoro mzito na mkubwa mno tangu walipoanza kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Maafa kwa Wazayuni kutokana na kupigwa kwa makombora na wanamuqawama wa Palestina

 

Taarifa hiyo imesema hayo kuashiria wimbi la mashambulizi ya wanamapambano wa Palestina na hasira za vijana wenye ghera na mashujaa wa Palestina huko Quds katika kukabiliana na ukatili na jinai za Israel.

Sehemu nyingine ya taarifa rasmi ya jeshi la SEPAH imesema, kambi ya kupambana na Uzayuni pamoja na jamii ya kimataifa zina wajibu wa kukabiliana na madhara makubwa na hatari ya vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu vya utawala wa Kizayuni unaoua watoto wasio na hatia na unaoendesha operesheni ya kuiyahudisha Palestina na kuangamiza kizazi cha wakazi wa ardhi hizo.