May 13, 2021 02:16 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inakaribisha ushirikiano na Saudi Arabia na ulimwengu mzima wa Kiarabu.

Dk Muhammad Javad Zarif alisema hayo jana (Jumatano) mjini Damascus nchini Syria na kuongeza kuwa, Tehran ina matumaini kutakuwa na ushirikiano mzuri na wa nia njema kati yake na Saudi Arabia kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu nchini Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia mazungumzo yake na Rais Bashar al Assad wa Syria na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na kusema, katika mazungumzo yangu na Rais Bashar al Assad na pia Waziri Faisal Miqdad, tumejadiliana masuala muhimu ya pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa.

Watoto wa Yemen wako katika hali mbaya. Iran daima imekuwa ikisisitiza iko tayari kushirikiana na nchi yoyote ikiwemo Saudi Arabia kuwapunguzia mateso watoto wa Yemen

Ameashiria pia umuhimu wa uchaguzi ujao nchini Syria na kusema kuwa, Tehran na Damascus zina msimamo mmoja katika suala zima la kuimarisha amani, usalama na utulivu pamoja na kuiletea ustawi na maendeleo Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia pia jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa mji wa Quds na Ukanda wa Ghaza na kusema, nimefanya mazungumzo na viongozi wa Syria kuhusu Palestina na njia za kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni pamoja na umuhimu wa jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ya kuwalinda wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Vile vile amesisitiza kuwa, jinai za Israel zitaendelea kukabiliwa na muqawama wa kishujaa wa wananchi wa Palestina na kwamba ni jukumu la jamii ya kimtaifa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda wananchi madhlumu wa Palestina.

Tags