May 13, 2021 11:43 UTC
  • Rais Rouhani: OIC inapaswa kuwa amilifu zaidi katika kadhia ya Palestina

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kuwa amilifu zaidi na kutekeleza ipasavyo jukumu lake kuhusu kadhia ya Palestina na hasa katika matukio ya hivi sasa.

Rais Rouhani amesema hayo leo Alkhamisi katika mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani ambapo mbali na kutoa mkono wa baraka za Idul Fitr kwa serikali na wananchi wa Qatar, ameipongeza Doha kwa msimamo wake wa kulaani jinai za hivi sasa za Wazayuni kwenye Msikiti wa al Aqsa na mashambulizi ya kikatili ya Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Kwenye mazungumzo hayo ya simu, Rais Rouhani amesema: Nchi za Kiislamu zina wajibu wa kuungana na kushirikiana katika kuwalinda wananchi wa Palestina, kuikomboa nchi yao na kukabiliana na uvamizi na vitendo vya kiuadui na kibaguzi vya utawala wa Kizayuni.

Israel inafanya mauaji ya kimbari Palestina

 

Kwa upande wake, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani ametoa mkono wa baraka za Idul Fitr kwa serikali na wananchi wa Iran na kupongeza msimamo imara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu matukio ya hivi sasa huko Palestina.

Amesema, Qatar ina msimamo mmoja na Iran katika suala zima la kulaani jinai za Wazayuni na kupigania kukomeshwa haraka iwezekanavyo mashambulio dhidi ya Wapalestina. Vile vile ameitaka OIC kutoa mchango mkubwa zaidi katika suala hilo.

Mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu umeshuhudia ongezeka la kutisha la jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa maeneo tofauti hasa ya Quds na Ukanda wa Ghaza. Hadi hivi sasa makumi ya Wapalestina wameshauliwa shahidi na wanajeshi magaidi wa Israel.